Jaribio la Wazayuni la kumuua kigaidi Mkuu wa Majeshi ya Yemen lagonga mwamba
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti habari ya kufeli jaribio la utawala haramu wa Israel la kumuua Mkuu wa Majeshi ya Yemen, kwa mara ya pili sasa.
Tovuti ya Walla ya Israel imeripoti habari ya kugonga mwamba jaribio la kumuua kigaidi Meja Jenerali Mohammed Abdul Karim al-Ghamari, Mkuu wa Majeshi ya Yemen na kueleza kuwa, kwa mujibu wa duru za usalama, operesheni hiyo ilitekelezwa lakini kamanda huyo alinusurika katika jaribio hilo la mauaji la utawala wa Israel.
Vyombo vya habari vya Israel pia vimesema kuwa, Tel Aviv inazingatia jibu la kijeshi katika kukabiliana na mashambulizi ya makombora yanayoendelea kutoka Yemen.
Kwa mujibu wa duru za habari, jeshi la Kizayuni linalokalia kwa mabavu ardhi za Waislamu na Waarabu Asia Magharibi na shirika lake la kijasusi la Mossad yanajiandaa kulenga vituo muhimu vinavyofungamana na Harakati ya Ansarullah ya Yemen.
Hii si mara ya kwanza kwa vyombo vya habari vya Israel kuripoti jaribio la kutaka kumuua Mkuu wa Majeshi ya Yemen. Hapo awali, wakati wa vita vya siku 12 vya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jeshi la Anga la Israel lilijaribu kumuua Meja Jenerali al-Ghamari bila mafanikio.
Haya yanaripotiwa huku vyombo vya habari vya Yemen vikiripoti habari ya kushtadi mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel yakilenga maeneo ya kusini na magharibi mwa Sana’a, mji mkuu wa Yemen.
Marekani na Israel zimekuwa zikiishambulia Yemen kwa sababu tu nchi hiyo maskini ya Kiarabu imesimama kidete kuushinikiza utawala wa Kizayuni usitishe vita vyake vya mauaji ya halaiki dhidi ya Gaza.