Hamas, Jihadul Islami zalaani uvamizi wa kifashisti wa Israel dhidi ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129982-hamas_jihadul_islami_zalaani_uvamizi_wa_kifashisti_wa_israel_dhidi_ya_yemen
Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina za Hamas na Jihadul Islami zimeshutumu vikali mashambulizi mabaya ya Israel dhidi ya mji mkuu wa Yemen na miundombinu ya kiraia, na kuyaelezea kama "ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa" na gharama ya kuilinda Palestina.
(last modified 2025-08-25T10:44:56+00:00 )
Aug 25, 2025 10:44 UTC
  • Hamas, Jihadul Islami zalaani uvamizi wa kifashisti wa Israel dhidi ya Yemen

Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina za Hamas na Jihadul Islami zimeshutumu vikali mashambulizi mabaya ya Israel dhidi ya mji mkuu wa Yemen na miundombinu ya kiraia, na kuyaelezea kama "ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa" na gharama ya kuilinda Palestina.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumapili, Hamas imesisitiza kuwa, "uchokozi wa kifashisti" wa Israel dhidi ya Yemen ulikuwa na lengo la kuwazuia wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu kuwaunga mkono Wapalestina.

"Uchokozi wa kigaidi wa Wazayuni dhidi ya Yemen, unaolenga maeneo ya makazi na raia, ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kujitawala nchi za Kiarabu na sheria za kimataifa," imesema taarifa hiyo ikiongeza kuwa, "Uchokozi huu wa kifashisti unalenga kuzuia Yemen kusaidia wananchi madhulumu wa Palestina." 

Kundi hilo la Muqawama lenye makao yake Gaza limesisitiza kwamba, uvamizi huo unahitaji msimamo thabiti wa Waarabu na Waislamu katika kuunga mkono Yemen, na mshikamano na watu wa Palestina dhidi ya ukatili wa Wazayuni na malengo yake ya kikoloni, hasa baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjami Netanyahu kueleza waziwazi nia yake ya kutimiza njozi ya "Israel Kubwa Zaidi" kwa kupora ardhi za Waarabu.

Kadhalika Hamas imetoa wito kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, pamoja na vikosi vyote huru, "kujiunga na njia hii ya heshima kwa ajili ya kukomesha uvamizi na kukomboa maeneo yetu matakatifu na ardhi zetu zote za Kiarabu zinazokaliwa kwa mabavu."

Katika taarifa tofauti, Jihadul Islami pia imelaani hujuma ya Israel dhidi ya miundombinu ya kiraia na kulengwa kwa viongozi wa Yemen. Kundi hilo la Muqawasma limebaini kuwa, mashambulizi hayo ni uhalifu wa kivita ambao Marekani inaunga mkono kikamilifu.

"Watu wa Yemen wanalipa gharama kwa msimamo wao thabiti wa kuwaunga mkono watu wa Palestina na kwa juhudi zao za kukomesha uhalifu katika Ukanda wa Gaza," imeongeza taarifa hiyo.

Haya yanaripotiwa huku vyombo vya habari vya Yemen vikiripoti habari ya kushtadi mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel yakilenga maeneo ya kusini na magharibi mwa Sana’a, mji mkuu wa Yemen. Jana Jumapili, Israel ilifanya mashambulizi ya anga katika eneo la Sana’a nchini Yemen siku ya Jumapili na kuua takriban watu sita na wengine 86 kujeruhiwa.