Taarifa ya mwisho ya mkutano wa OIC yapinga mpango wa "Israel Kubwa"
Taarifa ya mwisho ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imesisitiza upinzani dhidi ya matamshi ya kutowajibika ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuhusu dira ya "Israel Kubwa."
Taarifa hiyo inasema: "Tunalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya mkutano kuhusu ukiukaji wa haki unaofanywa dhidi ya watu wa Palestina."
Taarifa hiyo imeunga mkono juhudi za usitishaji vita huko Gaza na kulaani ukaidi wa Israel na upinzani wake dhidi ya juhudi za kupatikana amani katika eneo hilo la Palestina.
Vilevile imetoa wito wa kufunguliwa vivuko vya kuingia Gaza na kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hilo kwa wingi na bila vikwazo.
Sehemu moja ya taarifa ya mwisho ya mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu uliofanyika Jeddah nchini Saudi Arabia imesema: "Tunaka dhamana ya uhuru wa utekelezaji wa mashirika ya misaada huko Gaza, yanaoongozwa na shirika la UNRWA."
Nchi zilizoshiriki katika mkutano huo zimesisitiza katika taarifa yao ya mwisho kwamba: Tunapinga matamshi ya kutowajibika yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuhusu mpango unaoitwa "Israel Kubwa", na imelaani vikali mauaji ya waandishi habari katika Ukanda wa Gaza.
Mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Kiislamu (OIC) ulianza Jumatatu mjini Jeddah, Saudi Arabia.
Lengo la mkutano huu lilikuwa kuchunguza njia za kukabiliana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Akihutubia katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kimataifa kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel yanayoendelea huko Gaza, akisema kuwa nchi zote zinapaswa kusimama upande sahihi wa historia ambao "hautasamehe" ucheleweshaji wowote zaidi wa kupunguza mateso ya watu wa Palestina.