Hamas: Hakuna shaka Marekani imehusika na shambulio la Doha
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani vikali ushirikiano wa Marekani na Israel katika shambulizi la anga dhidi ya Qatar na jaribio la mauaji dhidi ya viongozi wa kundi hilo hilo la kupigania ukombozi wa Palestina, ikisisitiza kuwa Washington na Tel Aviv zinataka kusambaratisha mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Msemaji wa Hamas, Fawzi Barhoum amesema kwamba, jaribio la kuua timu ya mazungumzo ya Hamas huko Doha, pamoja na vitisho vinavyoendelea vya kushambulia uongozi wa harakati hiyo nje ya nchi, vinaonyesha Israel "kutoweza kufikia malengo yake" baada ya miezi 23 ya vita dhidi ya Gaza.
Barhoum ameeleza bayana kuwa, jaribio hilo la mauaji ya kigaidi lilitokea wakati ujumbe huo wa Hamas ulikuwa katika mazungumzo kuhusu pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano Gaza.
Msemaji wa Hamas amebainisha kuwa, shambulio hilo lililenga makazi ya mkuu wa jumbe wa mazungumzo Khalil al-Hayya, na kumjeruhi mke wake, mke wa mtoto wake aliyeuawa shahidi, Hammam al-Hayya, pamoja na wajukuu zake. Amesema "Uhalifu huo" umefanywa katikati ya mchakato mzima wa mazungumzo.
Afisa huyo wa Hamas amesema kuwa, shambulio la Israel haliashirii tu shambulio dhidi ya mamlaka na usalama wa Qatar, bali pia ni "tangazo la vita vya wazi dhidi ya mataifa yote ya Kiarabu na Kiislamu" na tishio kwa uthabiti wa eneo zima la Asia Magharibi.
Barhoum ameijia juu Washington kwa kuwa "mshirika kamili" wa shambulio hilo la kichokozi la Israel. Ikulu ya White House ilidai kuwa Rais Donald Trump wa Marekani hakukubaliana na uamuzi wa Israel wa kuchukua hatua za kijeshi.
Trump anadai kuwa hakuarifiwa mapema na alipopata habari hizo, alimwomba mjumbe wake maalum, Steve Witkoff, kuipa Qatar tahadhari mara moja - lakini shambulio lilikuwa tayari limeshaanza.