Hamas: Msimamo mmoja wa Muqawama wa Palestina umeitenga zaidi Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i131702-hamas_msimamo_mmoja_wa_muqawama_wa_palestina_umeitenga_zaidi_israel
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema msimamo mmoja ulioidhinishwa na mirengo yote ya Muqawama wa Palestina kuhusu pendekezo la Rais wa Marekani la kusitisha mapigano Gaza, umepelekea kuzidi kutengwa Israel kimataifa.
(last modified 2025-10-07T06:11:44+00:00 )
Oct 07, 2025 06:11 UTC
  • Hamas: Msimamo mmoja wa Muqawama wa Palestina umeitenga zaidi Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema msimamo mmoja ulioidhinishwa na mirengo yote ya Muqawama wa Palestina kuhusu pendekezo la Rais wa Marekani la kusitisha mapigano Gaza, umepelekea kuzidi kutengwa Israel kimataifa.

Msemaji wa Hamas, Jihad Taha alisema hayo jana Jumatatu na kusisitiza kuwa, msimamo huo wa pamoja wa mhimili wa Muqawama umejengeka katika misingi ya maslahi ya watu wa Palestina.

"Tunakaribisha msimamo wa Waarabu na wa kimataifa unaounga mkono haki ya Palestina na ushiriki mzuri wa pande zinazopinga kukomesha uchokozi," Taha amesema na kueleza kuwa, Israel lazima ijitolee kikweli kusitisha uvamizi wake, lakini kuendelea kwa jinai zake kunadhihirisha uwongo wa msimamo wake uliotangaza kuhusu mpango huo wa amani wa Gaza.

Msemaji wa Hamas amesisitiza kwamba, Gaza ni "sehemu muhimu ya ardhi ya Palestina, na utawala wake lazima uzingatie makubaliano ya kitaifa ya Palestina."

Matamshi yake yametolewa wakati wajumbe wanaoiwakilisha Israel na Hamas wakiendelea na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Misri kuhusu mpango huo uliopendekezwa na Marekani wa kusitisha mapigano Gaza.

Siku ya kwanza ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Hamas nchini Misri hiyo jana ilimalizika kwa 'hali chanya', huku kukiwa na matumaini ya uwezekano wa kuidhinishwa kwa mpango wa Trump wenye vipengele 20 wa kumaliza vita dhidi ya Gaza.

Vyanzo vya habari vimeiambia kanali ya Al Jazeera ya lugha ya Kiarabu kwamba, mkutano katika mji wa kitalii wa Sharm el-Sheikh jana Jumatatu ulikuwa "chanya" na kwamba ramani ya njia iliandaliwa kwa jinsi mazungumzo ya sasa yatakavyoendelea. Wapatanishi wanatazamiwa kuendelea na majadiliano zaidi leo Jumanne.