UNICEF yaonya kuhusu mlipuko wa magonjwa miongoni mwa watoto Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134286-unicef_yaonya_kuhusu_mlipuko_wa_magonjwa_miongoni_mwa_watoto_gaza
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeonya juu ya ongezeko la hatari ya milipuko ya magonjwa miongoni mwa watoto katika Ukanda wa Gaza, huko Palestina.
(last modified 2025-12-14T07:11:14+00:00 )
Dec 14, 2025 07:11 UTC
  • UNICEF yaonya kuhusu mlipuko wa magonjwa miongoni mwa watoto Gaza
    UNICEF yaonya kuhusu mlipuko wa magonjwa miongoni mwa watoto Gaza

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeonya juu ya ongezeko la hatari ya milipuko ya magonjwa miongoni mwa watoto katika Ukanda wa Gaza, huko Palestina.

Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa yake kwamba, sambamba na kuendelea hali mbaya ya hewa afya ya watoto inazidi kuwa hatarini, na ucheleweshaji wa kuwasili kwa vitu muhimu umeongeza zaidi hatari.

UNICEF imetoa wito wa kuongezwa mara moja kwa misaada ya kibinadamu, hasa mavazi ya majira ya baridi na vifaa vya makazi ya dharura, na kusisitiza haja ya kuhakikisha kunakuwepo na harakati za misaada zilizo salama, za haraka na zisizozuiliwa, ikiwa ni pamoja na kiasi kikubwa cha vifaa vya majira ya baridi vinavyorundikwa kwenye mpaka wa Gaza.

Kulingana na tathmini ya lishe iliyofanywa na UNICEF na washirika wake mwezi uliopita wa Novemba, karibu watoto 9,300 walio chini ya miaka mitano huko Gaza wanakabiliwa na utapiamlo mkali.

Kwa upande wake, Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema kwamba zaidi ya watu 140,000 wameathiriwa na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko katika maeneo zaidi ya 200 ya wakimbizi katika Ukanda wa Gaza.

Farhan Haq amesisitiza udharura wa kuondoa vikwazo vya kuingizwa misaada katika ukanda huo, akitilia mkazo ulazima la kuondoa marufuku ya kazi ya Shirika la Misaada na Kazi la Umoja wa Mataifa kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA).