Ulimwengu unasubiri siku ya ghadhabu duniani kuunga mkono wafungwa wa Kipalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i135938-ulimwengu_unasubiri_siku_ya_ghadhabu_duniani_kuunga_mkono_wafungwa_wa_kipalestina
Kampeni za kimataifa na za haki za binadamu zimetoa wito kwa watu huru duniani kote kushiriki katika mkusanyiko mkubwa wa kimataifa tarehe 31 Januari kwa ajili ya kuwaunga mkono Wafungwa wa Kipalestina.
(last modified 2026-01-26T23:03:40+00:00 )
Jan 26, 2026 23:03 UTC
  • Ulimwengu unasubiri siku ya ghadhabu duniani kuunga mkono wafungwa wa Kipalestina

Kampeni za kimataifa na za haki za binadamu zimetoa wito kwa watu huru duniani kote kushiriki katika mkusanyiko mkubwa wa kimataifa tarehe 31 Januari kwa ajili ya kuwaunga mkono Wafungwa wa Kipalestina.

Lengo la mkusanyiko huo ni kuvunja kimya cha kimataifa juu ya kuongezeka mateso ya wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Israel, ukiukwaji wa haki za binadamu, mateso, kutengwa, na kunyimwa haki za msingi zaidi za binadamu.

Wito huu ni sehemu ya harakati za Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Wafungwa wa Kipalestina, ambayo inatekelezwa kwa hima na juhudi ya Kampeni ya Kimataifa ya Kuokoa Wafungwa kwa ushirikiano na Kampeni ya Utepe Mwekundu ndani ya mfumo wa harakati za kimataifa. Lengo lake ni kuunganisha harakati za kimataifa za kuwaunga mkono wafungwa na kufichua jinai za kupangwa za utawala wa Kizayuni ndani ya jela za utawala huo ghasibu.

Kampeni hizi mbili zimeitisha maandamano, mikusanyiko, na harakati za wananchi katika miji mbalimbali duniani kote ili kusisitiza ukweli kwamba suala la wafungwa wa vita lipo katika akili na dhamiri za watu huru kote ulimwenguni. Taarifa ya waandaaaji wa kampeni hii wanasema, lengo ni kuishinikiza jamii ya kimataifa kukubali majukumu yake ya kisheria na ya kibinadamu kuhusiana na mateso ya wafungwa, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji, kifungo cha upweke, kunyimwa matibabu na kutoruhusiwa kutembelewa wafungwa na ndugu zao, na kupinga kushikiwa wanawake na watoto katika hali na mazingira mabaya na yasiyofaa kibinadamu.