Afisa wa Umoja wa Mataifa: Usitishaji mapigano Gaza si wa kweli
-
Philippe Lazzarini
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) amelaani shambulio la jeshi la Israel katika kitongoji cha Sheikh Radwan kaskazini magharibi mwa Jiji la Gaza, ambalo limeua makumi ya Wapalestina akisema kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano katika eneo hili si ya kweli.
"Kusitisha mapigano halisi kuna maana ya kusimamisha mauaji na kukomesha vita, lakini zaidi ya watu 500, wakiwemo watoto 100, wameuawa huko Gaza tangu utekelezaji wa makubaliano hayo ulipoanza Oktoba mwaka jana," amesema Philippe Lazzarini.
Ameongeza kuwa: "Wakazi wa Ukanda wa Gaza wanastahili makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yana maana ya kusimamishwa mauaji na kuandaa njia ya kukomesha vita."
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amelitaja shambulio la jeshi la Israel katika kitongoji cha Sheikh Radwan kaskazini magharibi mwa Jiji la Gaza jana Jumamosi, ambalo limeua zaidi ya Wapalestina 30, kuwa ni siku nyingine ya giza huko Gaza.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Ghaza imesema zaidi ya Wapalestina 500 wameuliwa shahidi na jeshi la utawala wa kizayuni tangu usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani huko Ghaza ulipoanza kutekelezwa Oktoba 10.
Vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala ghasibu wa Israel Oktoba 2023 dhidi ya Ghaza vimewaua watu wasiopungua 71,769 na kuwajeruhi 171,483.