Mpango wa hatua nne wa Netanyahu wa kuumeza Ukingo wa Magharibi
Uamuzi wa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu siku ya Jumapili kuhusu Ukingo wa Magharibi ulikuwa msumari wa mwisho katika jeneza la udanganyifu na matumaini ya wale waliofikiri kwamba chini ya kivuli cha makubaliano na wavamizi wa Kizayuni, inawezekana kupata haki za Wapalestina.
Muswada uliopasishwa na baraza la mawaziri la usalama la utawala ghasibu wa Israel linaloongozwa na Benjamin Netanyahu, kwa mhimili wa mawaziri wenye misimamo mkali kama vile Bezalel Smotrich na Israel Katz, umeelezewa na weledi wa masuala ya kisiasa na makundi ya Wapalestina kama msumari wa mwisho katika jeneza la Makubaliano ya Oslo. Maamuzi haya yanachukuliwa kuwa hatua ya moja kwa moja zaidi kuelekea kutekeleza njama za Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel za kumiliki kwa wigo mpana zaidi maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu na kurahisisha unyakuzi wa kivitendo wa Ukingo wa Magharibi.
Azimio la baraza la mawaziri la Israel linatokana na mihimili minne mikuu, ambayo kila moja kwa njia fulani unaendeleza lengo kuu la kuimarisha uwepo wa Wazayuni na kukomesha wazo la kuundwa taifa la Palestina. Mihimili hiyo ni:
Mosi, kufutwa sheria ya enzi ya Jordan ambayo ilikuwa imepiga marufuku uuzaji wa ardhi kwa Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi kwa miongo kadhaa.
Pili, kuondolewa mahitaji tata ya kiutawala na vibali maalum kwa miamala ya ardhi, na kufanya ununuzi wa ardhi na walowezi kuwa jambo rahisi na jepesi.
Tatu, kufufuliwa "Kamati ya Ununuzi wa Ardhi za Serikali," ambayo haikuwa ikifanya kazi kwa miaka mingi na sasa inaruhusu Israel kununua moja kwa moja ardhi kwa ajili ya upanuzi wa makazi.
Na nne, ni upanuzi mkubwa wa mamlaka ya utendaji ya taasisi za Israel katika Maeneo A na B chini ya udhibiti wa Mamlaka ya Palestina, katika maeneo nyeti kama vile mazingira, usimamizi wa maji, ulinzi wa mambo ya kale, na hata usimamizi wa maeneo ya kidini.
Kulingana na Israel Times, Mamlaka ya Ndani ya Palestina, inayoongozwa na Mahmoud Abbas, ilielezea maamuzi hayo katika taarifa kama "hatari," "haramu," na "jaribio la wazi la kuunganisha Ukingo wa Magharibi na kubadilisha muundo wa idadi ya watu."
Ofisi ya rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina pia iliiita hatua hiyo kuwa "muendelezo wa vita kamili dhidi ya watu wa Palestina" na utekelezaji wa kivitendo wa mipango ya uunganishaji ardhi na kuwafanya Wapalestina kuwa wakimbizi. Hussein al-Sheikh, naibu wa Mahmoud Abbas, pia alikiri waziwazi kwamba azimio tajwa "limeharibu karibu makubaliano yote ya awali."
Kwa upande mwingine, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imekiita kitendo hiki kuwa kielelezo cha wazi cha "uangamizaji kizazi" na "tishio la uwepo," na Hazem Qassem, msemaji wa harakati hiyo, amesisitiza haja ya umoja na kuimarishwa muqawama.
Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa wa Palestina pia imetathmini maamuzi haya kama "vitendo hatari zaidi tangu 1967" na kufikiwa kile kinachofahamika kama "msumari wa mwisho kwenye jeneza la Makubaliano ya Oslo."
Makundi ya Muqawama ya Palestina yamesisitiza katika taarifa kwamba, maamuzi mapya ya baraza la mawaziri la usalama la utawala wa uvamizi kuhusu Maeneo A na B ya Ukingo wa Magharibi yanamaanisha kuporwa eneo hilo, kuweka hali halisi mpya, na kukomesha uwepo wa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.
Muda wa kupitishwa kwa azimio hilo ambao umesadifiana na, usiku wa kuamkia ziara ya Netanyahu huko Washington, unaonyesha kwamba, Waziri Mkuu wa Israel hana wasiwasi sana kuhusu radiamali ya Marekani, mshirika wake wa muda mrefu. Imani hii imejikita katika historia dhahiri na ya kinafiki ya Marekani. Katika ngazi ya kauli na misimamo rasmi, maafisa wa Marekani, wakiwemo marais na maafisa wa serikali ya Washington siku zote wamekuwa wakiuita ujenzi wa vitongoji vya walowezi kuwa kinyume cha sheria na kikwazo cha amani, na wametangaza kupinga kwao uvamizi na unyakuzi. Hata hivyo, katika utendaji, Washington imekuwa mfuasi mkubwa na mwezeshaji wa mwendelezo na uimarishaji wa uvamizi kwa kutoa mabilioni ya dola katika misaada ya kijeshi kila mwaka, ambayo sehemu yake kubwa hutumika kulinda makazi na kuimarisha uwepo wa kijeshi katika Ukingo wa Magharibi, na kwa kutumia mara kwa mara haki yake ya kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia azimio lolote la kulaani Israel. Unafiki huu dhahiri umeunda mazingira ambayo yanampa ujasiri Netanyahu wa kuendeleza malengo yake ya uvamizi bila ya kuwa na woga.
Baada ya uvamizi wa Ukingo wa Magharibi na Baytul-Muqaddas Mashariki mwaka wa 1967, zaidi ya walowezi 700,000 wa Israel sasa wanaishi miongoni mwa Wapalestina wanaokadiriwa kuwa milioni tatu katika maeneo haya. Makazi hayo, ambayo yanachukuliwa kuwa kinyume cha sheria chini ya sheria ya kimataifa na yanachukuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa kikwazo kikuu cha suluhisho la mataifa mawili, kwani yanafanya umiliki wowote wa eneo kwa taifa la Palestina la baadaye kuwa jambo lisilowezekana. Shirika la Israel Peace Now pia limeonya kwamba uamuzi wa hivi karibuni utasababisha kufukuzwa zaidi Wapalestina, kwani baadhi ya makazi mapya yatajengwa kwenye ardhi iliyoporwa au katika maeneo yenye watu wengi wa Palestina, na hata kwenye vitongoji ambavyo watu wakazi wake waliondolewa huko mwaka 2005.