Hamas: Kamwe hatutakabidhi silaha zetu kwa Israel na Marekani
Naibu mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) nje ya nchi ametangaza kwamba harakati hiyo kamwe haitakabidhi silaha zake kwa Israel na Marekani.
Musa Abu Marzouk amesema katika mahojiano na shirika la habari la Urusi RIA Novosti kwamba: "Silaha zinaweza kukabidhiwa tu kwa upande wa Palestina, iwe ni Mamlaka ya Palestina au taifa la Palestina la baadaye, lakini kamwe hazitapelekwa kwa utawala wa Kizayuni, upande wowote wenye uhusiano nao, au kwa Marekani."
Hapo awali, Hossam Badran, mwanachama wa Idara ya Siasa ya Hamas, pia alitangaza kwamba suala la silaha linahusiana na haki za kisiasa na kitaifa za watu wa Palestina na haliko chini ya kundi lolote maalumu la muqawama la mapambano ya ukombozi.
Afisa mkuu wa Hamas ameongeza kuwa: "Silaha za kambi ya Muqawama na mapambano ya ukombozi zinahusishwa na haki ya watu wa Palestina kuanzisha taifa huru na kujitawala baada ya miongo kadhaa ya uvamizi."