Safari ya Waziri wa Ulinzi wa Russia mjini Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1741-safari_ya_waziri_wa_ulinzi_wa_russia_mjini_tehran
Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergey Shoigu ameitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kupanua zaidi wigo wa ushirikiano kati ya Moscow na Tehran katika masuala ya ulinzi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 22, 2016 16:41 UTC
  • Safari ya Waziri wa Ulinzi wa Russia mjini Tehran

Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergey Shoigu ameitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kupanua zaidi wigo wa ushirikiano kati ya Moscow na Tehran katika masuala ya ulinzi.

Shoigu ambaye aliwasili Tehran jana Jumapili amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa hapa nchini akiwemo Rais Hassan Rohani na Waziri mwenzake wa Ulinzi, Brigedia Jenerali Hussein Dehqan. Sergey Shoigu amemkabidhi rais Hassan Rohani ujumbe rasmi kutoka kwa Rais Vladimir Putin. Vile vile ametoa ripoti fupi kuhusu mwenendo wa mazungumzo ya Syria na hatua zilizopigwa na pande husika.

Mazungumzo ya Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergey Shoigu na mwenzake wa Iran, Hussein Dehqan yamejikita zaidi katika uhusiano wa kijeshi na kiulinzi wa nchi mbili hizi. Wawili hao wamezungumzia kwa kina utekelezwaji wa makubaliano ya pande mbili katika uwanja wa kijeshi na kusisitizia umuhimu wa kupanuliwa zaidi uhusiano wa Tehran na Moscow kwenye uga huo.

Safari ya Waziri wa Ulinzi wa Russia hapa nchini inafuatia ile ya Brigedia Jenerali Hussein Dehqan nchini Russia wiki iliyopita.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, ziara ya Shoigu hapa Tehran na ujumbe wa Rais Putin kwa mwenzake Hassan Rouhani wa Iran ni ishara ya kuweko ushirikiano wa karibu na wa kiistratejia kati ya Tehran na Moscow katika masuala ya kieneo na kimataifa, na pia inaonyesha jinsi Iran na Russia zilivyo na nafasi muhimu katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria. Kutokana na ukweli huo tunaweza kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zina mitazamo inayofanana katika masuala mengi ya kieneo na kimataifa. Hata katika kadhia ya Yemen, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, Russia kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inaweza kuwa na mchango wa aina yake katika kuishinikiza Saudi Arabia kukomesha mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya wananchi wa Yemen.

Huku Waziri wa Ulinzi wa Russia akifanya safari ya kikazi hapa mjini Tehran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amefika mjini Moscow na kukutana na mwenyeji wake, Sergei Lavrov. Mazungumzo ya Kerry na Lavrov yamegusia mazungumzo ya kujaribu kutafuta aina fulani ya usitishaji vita kati ya serikali na makundi hasimu huko Syria. Kerry amesema kuna matumaini ya kufikiwa makubaliano hayo ya usitishwaji vita katika siku chache zijazo lakini akasisitiza kuwa pande hasimu kwenye mgogoro wa Syria sharti zitumie makubaliano hayo kuanza mara moja mazungumzo ya amani.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa uhusiano wa kijeshi, kiulinzi, kisiasa na kiuchumi kati ya Iran na Russia ni wa muda mrefu na hilo linathibitishwa na safari zinazofanywa na maafisa waandamizi wa nchi mbili hizi katika miji ya Tehran na Moscow. Safari ya Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergey Shoigu hapa Tehran pia inatathminiwa katika kalibu hiyo hiyo.