Iran, Russia zajadili kuendeleza ushirikiano wa nyuklia
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amekutana na kuzungumza mjini Tehran na afisa wa ngazi ya juu wa Shirika la Taifa la Nishati ya Atomiki la Russia( Russia Rosatom) na kujadili kustawisha ushirikiano katika uga wa nishati ya nyuklia yenye malengo ya amani kati ya nchi mbili hizo waitifaki.
Mohammad Eslami jana alikuwa na mazungumzo hapa Tehran na Nikolai Spassky Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Nishati ya Atomiki la Russia anayehusika na masuala ya kimataifa.
Spassky amefanya ziara Tehran akiongoza ujumbe wa Russia kufuatia ziara iliyofanywa na Eslami huko Moscow Septemba 24 mwaka huu; ambapo pande mbili zilisaini makubaliano kwa ajili ya kushirikiana katika ujenzi wa viwanda vidogo vya nguvu za nyuklia (SMRs) nchini Iran.
Mkutano wa jana kati ya Eslami na Spassky ulijikita pia katika kujadili ushirikiano wa nyuklia kati ya pande mbili kupitia miradi inayolenga katika ujenzi wa viwanda vidogo vya nguvu za nyuklia.
Mohammad Eslami Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) na Nikolai Spassky Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Nishati ya Atomiki la Russia anayehusika na masuala ya kimataifa waligusia pia mkataba mwingine uliotiwa saini wakati wa ziara ya Eslami mjini Moscow kuhusu ushirikiano wa nchi mbili katika Mradi wa Kiwanda cha Nishati ya Nyuklia cha Hormoz unaojumuisha ujenzi wa vinu vinne vya kuzalisha umeme vya megawati 1,250.