Marais wa Iran na Russia wazungumzia hali ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1879-marais_wa_iran_na_russia_wazungumzia_hali_ya_syria
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, usitishaji vita nchini Syria haupaswi kuwe fursa ya kuwawezesha magaidi kujiimarisha nchini himo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 25, 2016 01:24 UTC
  • Marais wa Iran na Russia wazungumzia hali ya Syria

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, usitishaji vita nchini Syria haupaswi kuwe fursa ya kuwawezesha magaidi kujiimarisha nchini himo.

Rais Rouhani ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Rais Vladmir Putin wa Russia Jumatano ya jana ambapo walizungumzia suala la usitishaji vita nchini Syria na kuanza kufikisha misaada kwa raia na kuitaja hatua hiyo kuwa chanya.

Kwa mujibu wa marais wa Iran na Russia, hatua hiyo utakuwa na maslahi kwa wananchi wa Syria na kuonya kwamba mwenendo huo wa usitishaji vita wa muda, haupaswi kuwa fursa ya kuwapa mwanya magaidi kwa ajili ya kupokea misaada ya kifedha na silaha kutoka kwa waungaji mkono wao.

Sanjari na kusisitiza udharura wa kupambana na magaidi, Rais wa Iran amesema kuwa, mwenendo wa kusitisha vita nchini Syria unatakiwa uende sambamba na kuwafikishia misaada raia wa nchi hiyo chini ya idhini kamili ya serikali ya Damascus, kuwaachilia huru mateka na watu wasio kuwa na hatia na kudhibiti kikamilifu mipaka ya nchi hiyo.

Kwa upande wake Rais Vladmir Putin wa Russia ameashiria nukta muhimu zilizomo kwenye makubaliano ya usitishaji vita nchini Syria na kusema kuwa Russia inahitajia ushirikiano na uhusiano mpana ma Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vilevile ametilia mkazo suala la kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Syria na kulindwa ardhi yote ya nchi hiyo na kusema kuwa, mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi na kitakfiri ya Daesh, Jab'hatu Nusra na makundi mengine ya kigaidi yataendelea. Usitishaji vita nchini Syria umepangwa kuanza tarehe 27 mwezi huu katika fremu ya makubaliano ya Marekani na Russia.