Utawala wa Saudia na uenezaji ugaidi nje ya nchi
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imetangaza kuwa maelfu ya raia wa nchi hiyo wanashiriki kwenye harakati za makundi ya kigaidi nje ya nchi hiyo. Mansour Turki, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia alitangaza siku ya Jumatatu kuwa zaidi ya raia elfu mbili wa nchi hiyo wamejiunga na makundi ya kigaidi. Turki amesisitiza kuwa sehemu hasa walipo akthari ya watu hao zimeshajulikana.
Afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia amebainisha kuwa mamia ya raia wa Saudia wanashikiliwa kwenye jela za nje ya nchi hiyo kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya kigaidi.
Mansour Turki amefafanua kuwa jumla ya raia 1,540 wa Saudia wamejiunga na makundi ya kigaidi katika nchi za Syria, Afghanistan na Iraq.
Hata hivyo kabla ya takwimu hizo zilizotolewa na afisa huyo wa Saudia, ripoti mbalimbali zimeonyesha kuwa nchi hiyo ni moja ya waungaji mkono wakubwa na waenezaji wakuu wa fikra za kigaidi duniani.
Tukiziangalia harakati za utawala wa Aal Saud ndani na nje ya Saudia tutabaini kuwa aghalabu ya magaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa jumla wana asili ya nchi hiyo au wameathiriwa na mielekeo ya Uwahabi ambao chimbuko lake ni Saudi Arabia; na wanasaidiwa kwa fedha na silaha na utawala huo wa Riyadh. Chimbuko la kifikra la mitandao ya kigaidi ni mielekeo ya kufurutu mpaka na ya upotofu ya tapo la Uwahabi; na fikra hizo potofu zina nafasi muhimu katika kujitokeza harakati za kigaidi za Aal Saud katika eneo na kwengineko duniani. Kama ambavyo hivi sasa matawi ya magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia kama Daesh na Al-Qaeda yanaendesha harakati zao kwa majina tofauti kama Ansarush-Shariah, Boko Haram na Al-Shabaab barani Afrika, Asia na hata katika bara la Ulaya; na hii ni kengele ya hatari kwa usalama wa dunia.
Kwa mujibu wa moja ya nyaraka za mtandao wa Wikileaks, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Cliton amekiri kuwa Saudi Arabia ndiye mdhamini mkuu wa kifedha wa makundi ya kigaidi duniani. Katika nyaraka hizo Bi Hillary Clinton ameitaja Al-Qaeda, Taliban na kundi la Lashkar-Tayyibah la Pakistan kuwa ni miongoni mwa makundi maarufu ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudia na akatahadharisha kwamba Aal Saud ni wafadhili wa kifedha magaidi duniani.
Hii ni katika hali ambayo, akthari ya watuhumiwa wa mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 pia walikuwa na asili na uraia wa Saudia. Hata kufutwa kwa kurasa 28 za ripoti ya mashambulio hayo zinazoashiria kuhusika Saudi Arabia katika tukio hilo la kigaidi ni ithbati ya kuhusika moja kwa moja utawala wa Aal Saudi katika kuunga mkono ugaidi; hata hivyo kwa sababu ya uhusiano na ushirikiano wake na Riyadh, serikali ya Washington ilipinga kuwekwa wazi kuhusika huko kwa Saudia katika mashambulio ya Septemba 11, mwaka 2001. Imeelezwa kuwa katika taarifa zilizofichwa kwenye ripoti hiyo ni kutajwa moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA). Hatua hizo zinazidi kuweka nafasi ya Saudi Arabia katika mashambulio ya Septemba 11 na kuwa na taarifa CIA kuhusu hatua za Riyadh katika eneo na uundaji wake wa makundi ya kigaidi.
Leo hii hakuna asiyejua kama utawala wa Saudia, ni chimbuko la fikra za Uwahabi na muenezaji ugaidi katika maeneo tofauti duniani kuanzia Afghanistan hadi Marekani; na kutiwa nguvuni mamia ya raia wa Saudia katika nchi za Syria, Iraq, Yemen, Marekani na Ulaya ni ushahidi unaotilia nguvu hoja hiyo. Hakuna shaka yoyote kuwa kama si misaada ya nchi zenye fikra mgando za eneo hususan Saudi Arabia pamoja na madola ya Magharibi, makundi ya kigaidi yasingeweza kuendesha harakati zao kwa mapana na marefu kama inavyoshuhudiwa. Harakati za magaidi wa kitakfiri hazijakomea katika nchi za Syria na Iraq pekee lakini zinashuhudiwa pia katika nchi nyingine kadhaa za kaskazini mwa Afrika kama Misri, Libya na Tunisia. Usafirishaji na usambazaji ugaidi nje ya nchi inaweza kutajwa kuwa kazi ya pili kubwa inayofanywa na utawala wa Aal Saud baada ya usafirishaji mafuta. Na kutokana na hatua haribifu zinazofanywa na Aal Saud, Saudi Arabia imegeuka kuwa moja ya wafadhili na waungaji mkono wakubwa wa fikra za kigaidi duniani…/