Jumamosi, 6 Septemba, 2025
Leo ni Jumamosi 13 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 6 Septemba 2025 Miladia
Katika siku kama ya leo miaka 1157 alizaliwa Qadhi Jorjani maarufu kwa lakabu ya Abulhassan, faqihi, mwandishi na malenga wa Kiislamu. Jorjani alifunzwa masomo hayo ya kidini na Qadhi Mkuu wa mji wa Rey ulioko karibu na Tehran ya leo. Qadhi Jorjani ameandika vitabu vingi na miongoni mwake ni "Tafsirul Qur'an" na "Tahdhib al Tarikh". Qadhi Jorjani alifariki dunia mwaka 366 Hijria huko Neishabur na akazikwa huko Jorjan au Gorgan ya leo kaskazini mashariki mwa Iran.

Siku kama ya leo miaka 259 iliyopita, alizaliwa John Dalton, msomi na mtaalamu wa fizikia wa Kingereza katika familia ya watu wa kijijini. Kutokana na Dalton kupendelea sana elimu na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi, alifanikiwa kwenda shuleni na kujifunza mambo mbalimbali. Ni wakati huo ndipo alipoanza kufanya uchunguzi na utafiti katika masuala mbalimbali ya kielimu. Dalton alibuni na kuvumbua mambo mengi katika uwanja wa fizikia, kemia na sayansi asilia baada ya utafiti mkubwa.

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, jeshi la India lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Pakistan kufuatia machafuko ya zaidi ya mwezi mmoja katika mipaka ya nchi mbili hizo. Hivyo vilikuwa vita vya pili vikubwa kuwahi kutokea kati ya nchi mbili hizo jirani kuhusiana na eneo la Kashmir. Vita hivyo viliendelea kwa takribani wiki tatu. Pakistan na India zilikubaliana kusimamisha mapigano kufuatia upatanishi wa Urusi ya zamani. Viongozi wa nchi mbili hizo hatimaye waliafikiana kuanza mazungumzo tarehe 10 mwezi Juni mwaka 1966 huko Tashkent mji mkuu wa Uzbekistan nchini ya upatanishi wa Waziri Mkuu wa Urusi ya zamani. Japokuwa azimio la Tashkent lilibainisha njia za kumaliza mgogoro wa eneo la Kashmir na namna ya kuboresha uhusiano kati ya New Delhi na Islamabad na pia kukaribishwa na nchi mbalimbali duniani, lakini lilishindwa kumaliza hitilafu kati ya India na Pakistan kuhusu umiliki wa eneo la Kashmir.

Katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Eswatini (Swaziland zamani) ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na kila inapowadia siku kama ya leo husherekewa nchini humo kwa anwani ya siku ya taifa. Kuimarika ukoloni wa Ulaya huko kusini mwa Afrika kulisababisha pia Eswatini kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Ulaya. Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika ilipata uhuru. Eswatini ina ukubwa wa kilomita mraba 17364 na kijiografia iko kusini mwa bara la Afrika ikiwa inapakana na nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, kulifanyikka maandamano makubwa katika maeneo mengi ya Iran. Maandamano hayo yalifanyika kufuatia kilele cha mapambano ya Waislamu na wanamapinduzi wa Iran dhidi ya utawala dhalimu wa Shah. Kutokana na hali hiyo, serikali ya Shah, kwa kuogopa harakati ya wananchi ilipiga marufuku maandamano yoyote. Lakini wakati huo huo, Imam Khomeini (RA), Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akiwa Najaf, Iraq, alitoa tangazo na kuwataka wananchi kuendelea na mapambano yao.
