Kushtadi jinai za Israel na mashtaka yanayoongezeka dhidi ya Netanyahu
Jumanne ya wiki hii, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel alisisitiza kuwa, kuitambua rasmi Israel kama “Dola la Kiyahudi” utakuwa mwanzo mpya wa amani na Wapalestina na hatua moja mbele kuelekea katika kupatikana amani katika Mashariki ya Kati.
Akizungumza na vyombo vya habari Netanyahu alidai kwamba, upinzani wa siku zote wa Wapalestina juu ya suala la kuitambua rasmi Israel kwa anwani ya Dola la Kiyahudi katika mipaka yoyote ile, ndio chanzo kikuu cha mivutano. Madai ya Netanyahu yenye lengo la kuzipotosha fikra za waliowengi ulimwenguni kuhusiana na sababu ya mgogoro wa Palestina yanatolewa katika hali ambayo, wasababishaji wakuu wa mgogoro huo ni wavamizi wa Kizayuni na siasa za kupenda kujitanua za utawala wa kibaguzi wa Israel.
Matamashi haya ya Benjamin Netanyahu yanaonesha kuweko duru mpya ya harakati za Israel za kutaka kutambuliwa utawala huo ghasibu kama Dola la Kiyahudi ili kwa njia hiyo utawala huo uweze kusukuma mbele gurudumu la siasa zake za kutaka kujitanua na kuimarisha uvamizi wa utawala huo katika maeneo ya Wapalestina. Ukweli wa mambo ni kuwa, suala la kutaka kutambuliwa Israel kuwa ni dola la Kiyahudi daima umekuwa ni mpango wa ramani ya njia ya Wazayuni ambayo haina lengo jingine bighairi ya kufuatilia siasa zao za kupenda kujitanua na za kibaguzi. Daima viongozi wa Israel wamekuwa wakitafuta fursa ya kufanikisha hilo na kwa muktadha huo, waweze kupora na kukanyaga kikamilifu haki za Wapalestina.
Aidha hatua za Israel za kushadidisha ukandamizaji wake katika Mashariki ya Kati sanjari na kuzusha woga na hofu katika ardhi za Palestina umekuwa na lengo la kutwisha na kulazimisha mipango yake ya kupenda kujitanua ikubaliwe na Wapalestina. Ukweli wa mambo ni kuwa, hatua hizo zinafanyika ili kupoteza kabisa fursa ya kuundwa nchi ya Palestina. Juhudi mpya za utawala haramu wa Israel za kutaka kupasisha sheria ya kwamba, Israel itakuwa dola la kaumu ya Mayahudi, zinaonyesha dhahir shahir kwamba, Tel Aviv ni utawala wa kibaguzi ambao umejengeka juu ya misingi ya ubaguzi wa kikaumu.
Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, suala la kutaka kutambuliwa Israel kama nchi ya Mayahudi ni kisingizio tu kinachotumiwa na utawala huo kwa minajili ya kupora zaidi na zaidi ardhi za Wapalestina na wakati huo huo kuzuia kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi zao za asili, hatua ambazo zitapelekea kufukuzwa kikamilifu wakazi wa Wapalestina katika ardhi zilizokaliwa kwa mabavu mwaka1948 ambao wanatambulika kama Waarabu wa Israel.
Siasa hizo za Israel zimepelekea kupungua mno jamii ya Wapalestina katika maeneo hayo.
Tunapotupia jicho matokeo ya mpango wa Benjamin Netanyahu wa kutambuliwa rasmi uundwaji wa dola la Kiyahudi inaweza kufahamika wazi kwamba, madai ya Waziri Mkuu huyo wa Israel kwamba, kukubaliwa mpango huo kutapelekea kufunguliwa ukurasa mpya wa amani, ni porojo tupu na kupiga domokaya. Ukweli wa mambo ni kuwa, mipango kama hiyo ya kibaguzi itapelekea kushadidishwa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, jinai ambazo zimewachosha walimwengu.
Katika uwanja huo, mahakama moja mjini Washington Marekani imemfungulia mashtaka Netanyahu na viongozi kadhaa wa Israel kwa kutenda jinai za kivita. Aidha baadhi ya watu wa karibu na rais wa sasa wa Marekani Donald Trump nao wamefunguliwa mashtaka kutokana na kuunga kwao mkono jinai za kivita dhidi ya Wapalestina na kutoa himaya ya kifedha kwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina.
Kupanuka wigo wa mashtaka dhidi ya Israel hadi katika madola ya Magharibi ambayo yanahesabiwa kuwa waungaji mkono wa Israel ni jambo linalobainisha kuchoshwa fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Magharibi na hatua za jinai za utawala huo ghasibu. Ukweli ni kuwa, fikra za waliowengi ulimwenguni zinataka kupandishwa kizimbani viongozi wabaguzi na watenda jinai wa utawala haramu wa Israel.