Assad: Ufaransa inabeba dhima ya mauaji ya raia nchini Syria
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema hatua ya Ufaransa ya kuyaunga mkono magenge ya kigaidi yanayoendesha harakati dhidi ya vikosi vya serikali ya Damascus na wananchi imechangia moja kwa moja mauaji ya raia katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Rais Assad ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Ufaransa ya TF1 na idhaa ya Europe 1 na kuongeza kuwa, tangu mwanzo, Ufaransa iliweka wazi sera yake kuwa inaunga mkono magenge ya kigaidi yanayopambana na vikosi vya serikali.
Amesema Ufaransa na Marekani zimekuwa zikitangaza wazi wazi kuwa zinayatumia silaha magenge ya kigaidi eti yenye msimamo wa wastani ya Syria.
Rais wa Syria amesema serikali imekuwa ikichukua tahadhari kubwa inapofanya mazungumzo na muamala wowote na viongozi wa Kimagharibi, kwa kuwa asubuhi wanasema hili na jioni wanasema jingine tofauti.
Kiongozi wa taifa wa Syria amekariri kuwa, mustakabali wa nchi hiyo utaamuliwa na wananchi wenyewe na wala sio madola ya Kimagharibi.
Wiki iliyopita Rais Bashar al-Assad wa Syria aliutaja muungano wa kijeshi wa Marekani unaodai kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh/ISIS nchini Syria kuwa ni muungano wa kinjozi na wa kuihadaa dunia na kusisitiza kwamba, harakati za kundi hilo la kigaidi zilipanuka na kupata nguvu kutokana na operesheni za muungano huo.