Wanawake wa Ghaza waandamana kuwaunga mkono mateka wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26472-wanawake_wa_ghaza_waandamana_kuwaunga_mkono_mateka_wa_palestina
Makumi ya wanawake wa Kipalestina wakazi wa Ukanda wa Ghaza wameandamana katika eneo hilo kuonyesha mshikamamo wao kwa mateka wanawake wa Kipalestina ambao wanashikiliwa katika jela za utawala haramu wa Kizayuni.
(last modified 2025-10-23T09:42:35+00:00 )
Mar 16, 2017 14:41 UTC
  • Wanawake wa Ghaza waandamana kuwaunga mkono mateka wa Palestina

Makumi ya wanawake wa Kipalestina wakazi wa Ukanda wa Ghaza wameandamana katika eneo hilo kuonyesha mshikamamo wao kwa mateka wanawake wa Kipalestina ambao wanashikiliwa katika jela za utawala haramu wa Kizayuni.

Shirika la habari la Anatolia limearifu leo kuwa wanawake walioshiriki kwenye maandamano hayo yaliyoitishwa na Taasisi ya Muhja al Quds yenye mfungamano na Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina, walifika hadi mbele ya ofisi ya Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu katika mji wa Ghaza. Katika maandamano hayo, wanawake hao wakazi wa Ukanda wa Ghaza walikuwa wamebeba mabango mbalimbali wakizitaka taasisi za kimataifa za kuteteta haki za binadamu kuchukua hatua ili kuulazimisha utawala wa Kizayuni uwaachilie huru mateka wanawake wa Kipalestina waliofungwa katika jela za Israel. 

Wanawake wa Kipalestina wakiandamana wakitaka kuachiwa huru wenzao waliotekwa na Wazayuni na kushikiliwa katika jela za kutisha za Israel

Tariq Abu Shuluf msemaji wa Kampeni wa Taasisi ya Muhja al Quds ameeleza kuwa: Wanawake wa Kipalestina ni nembo ya mapinduzi ya sasa ya Palestina na ni mashuhuda wa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni ndani ya jela zake hizo. Itafahamika kuwa, mateka wanawake wa Kipalestina hususan wale walio na watoto wanazuiwa kuonana na watoto wao na wanaishi katika hali ngumu katika jela za utawala wa Kizayuni. Jumla ya mateka wanawake wa Kipalestina 56, 12 kati yao wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 wamefungwa katika jela za utawala wa Kizayuni. Takwimu rasmi zilizotolewa na Palestina zinaonyesha kuwa  Wapalestina karibu elfu saba wanashikiliwa katika jela za Israel huku wakiishi katika hali mbaya na kunyima haki zao hata ndogo kabisa za kibinadamu.