Imarati yazidi kuimarisha uhusiano na utawala haramu wa Israel
Uhusiano wa kiraifiki baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu au Imarati na utawala wa Kizayuni wa Israel umezidi kufichuka baada ya kubainika kuwa pande hizo mbili zina miradi ya pamoja ya kiuchumi na zinafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi.
Shirika la Habari la Palestina limefichua kuwa, uhusiano wa Imarati na utawala wa Kizayuni umefika kiwango ambacho mji wa Abu Dhabi sasa umebadilika na kuwa kituo muhimu zaidi cha utawala wa Kizayuni katika nchi za Kiarabu. Israel inautumia mji wa Abu Dhabi kama kitovu chake cha masuala ya usalama, ujasusi na biashara katika nchi za Kiarabu.
Magazeti ya Kizayuni hivi karibuni yaliandika kuwa Imarati imetiliana saini mkataba na shirika la usalama la utawala wa Israel lijulikanalo kwa jina la AGT ambalo litakuwa na jukumu la kulinda mabomba na mafuta na gesi ya Imarati.
Nyaraka zilizofichuka zinaonyesha kuweko ushirikiano wa karibu baina ya Imarati na Israel katika kuuyahudisha mji wa Quds Tukufu, wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Tovuti ya Kimarekani ya Intercept juzi Jumamosi ilichapisha nyaraka za siri zinazoonyesha namna Yusuf al Otaiba balozi wa Imarati nchini Marekani alivyokuwa akishirikiana na maafisa wa Marekani kujaribu kuzuia kufanyika kikao cha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, mjini Doha, Qatar.