Qatar: Tangu awali tulipinga muungano wa Saudia wa kuishambulia Yemen
(last modified Wed, 19 Jul 2017 14:20:03 GMT )
Jul 19, 2017 14:20 UTC
  • Qatar: Tangu awali tulipinga muungano wa Saudia wa kuishambulia Yemen

Waziri wa Ulinzi wa Qatar amesema kuwa, tangu awali Doha ilipinga muungano unaoongozwa na Saudia katika kuishambulia kijeshi Yemen, kwani iliamini utatuzi wa mgogoro huo haukuwa wa kijeshi.

Khalid bin Mohammad Al Attiyah ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya TRT ya Uturuki ambapo pamoja na mambo mengine amesema kuwa, baadhi ya nchi za Kiarabu ziliishinikiza sana Qatar ijiunge na muungano huo wa Saudia kuishambulia Yemen, lakini Doha haikuwa tayari kufanya hivyo.

Sehemu ndogo tu ya jinai zinazofanywa na muungano wa Saudia dhidi ya Wayemen

Vita vya Saudia kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu pamoja na Marekani, Israel na nchi nyingine za Magharibi dhidi ya Yemen vilianza tarehe 26 Machi 2015 kwa lengo la kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu nafasi hiyo na kutoroka nchi. Katika hujuma hizo, Saudia na washirika wake waliizingira kila upande Yemen, mzingiro ambao unaendelea hadi sasa. Mashambulizi ya kila upande ya Saudia nchini Yemen yamesababisha zaidi ya watu elfu 13 kuuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa.

Bendera za baadhi ya nchi za Kiarabu zenye mzozo na Qatar

Kadhlika Saudia kwa kushirikiana na nchi tatu za Kiarabu, yaani Imarat, Bahrain na Misri zilikata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar hapo tarehe tano Juni mwaka huu kwa madai kuwa serikali ya Doha inaunga mkono ugaidi, hatua ambayo ilienda sambamba na kuiwekea mzingiro wa kila upande nchi hiyo ya Kiarabu.

 

 

Tags