Baada ya Saudia, Imarati nayo yazusha balaa, yataka HAMAS ipinduliwe Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i32020-baada_ya_saudia_imarati_nayo_yazusha_balaa_yataka_hamas_ipinduliwe_ghaza
Katika kile kinachoonekana wazi ni kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwasahulisha walimwengu jinai hizo, Umoja wa Falme za Kiarabu nao umetaka Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ipinduliwe katika Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Jul 20, 2017 07:56 UTC
  • Baada ya Saudia, Imarati nayo yazusha balaa, yataka HAMAS ipinduliwe Ghaza

Katika kile kinachoonekana wazi ni kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwasahulisha walimwengu jinai hizo, Umoja wa Falme za Kiarabu nao umetaka Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ipinduliwe katika Ukanda wa Ghaza.

Leo Alkhamisi, televisheni ya al Alam imemnukuu Dhahi Khalfan Tamim, Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi la Dubai akiiambia kanali ya lugha ya Kiarabu ya televisheni ya Sky News ya nchini Uingereza inayorusha matangazo yake kutokea Abu Dhabi kwamba, Imarati haiwezi kuwasaidia wananchi wa Ghaza madhali bado Harakati ya Mapambano ya Kiislamu HAMAS iko katika ukanda huo. 

Matamshi hayo ya kichokozi ya Umoja wa Falme za Kiarabu yamewakasirisha mno wananchi wa Palestina ambao wamesema wanasikitishwa mno na matamshi kama hayo kutoka kwa nchi ya Waarabu na Waislamu tena katika wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha jinai zake katika Msikiti wa al Aqsa na mji mtakatifu wa Quds.

Nembo ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS

Hivi karibuni pia, kitendo cha balozi wa Saudi Arabia nchini Algeria, Sami bin Abdullah al Saleh cha kuishambulia Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kudai kuwa eti ni harakati ya kigaidi inayopanga njama zake katika hoteli za nyota tano nchini Qatar, iliwakasirisha sana watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Algeria. 

Matamshi hayo ya Saudia na Imarati dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina yanatolewa wakati huu ambapo ulimwengu wa Kiislamu unahitajia mno umoja na mshikamano kwa ajili ya kupambana na jinai za kila namna za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya maeneo matakatifu ya Waislamu, kikiwemo Kibla chao cha kwanza, yaani Msikiti wa al Aqsa.