Israel yapinga kuundwa kamati ya kimataifa ya kuchunguza jinai za Gaza
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya utawala haramu wa Israel imepinga vikali uamuzi wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wa kutaka wachunguzi wa kimataifa wa jinai za vita wapelekwe haraka Ukanda wa Gaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu kufanya uchunguzi kuhusu mauaji ya kinyama ya Wapalestina yaliyofanywa na askari wa Israel.
Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Israel imedai kwamba, kwa mara nyingine Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limethibitisha kuwa, muundo wake uko dhidi ya Israel.
Sehemu nyingine ya taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya utawala ghasibu wa Israel imedai kwamba, matokeo ya uchunguzi wa kamati hiyo ya kutafuta ukweli ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa yanaeleweka wazi kabla hata ya kuanza uchunguzi wenyewe.
Siku ya Ijumaa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) lilipiga kura ya kutaka wachunguzi wa kimataifa wa jinai za vita wapelekwe haraka Ukanda wa Gaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu kufanya uchunguzi kuhusu mauaji ya kinyama ya Wapalestina yaliyofanywa na askari wa Israel.
Azimio lililopitishwa katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liliungwa mkono na nchi 29 wanachama na kupingwa na Marekani na Australia. Nchi nyingine 14 hazikupiga kura.
Wapalestina 106 wameuawa shahidi na askari wa utawala vamizi wa Israel, wakiwemo watoto 15 tangu maandamano ya Wapalestina ya "Haki ya Kurejea" yalipoanza tarehe 30 Machi. Wapalestina wengine zaidi ya 12,000 wamejeruhiwa katika kipindi hicho, huku Wapalestina 3,500 miongoni mwao wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi za moto na askari wa Kizayuni.