Qatar: Mliotuwekea vikwazo acheni ndoto za alinacha
(last modified Tue, 05 Jun 2018 14:03:22 GMT )
Jun 05, 2018 14:03 UTC
  • Qatar: Mliotuwekea vikwazo acheni ndoto za alinacha

Katika hali inayoonekana ni ya kutoweka matumaini ya kutatuliwa hivi karibuni mgogoro wa Qatar na nchi nne za Kiarabu, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo amesema katika kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Doha ianze kuwekewa vikwazo, kwamba nchi nne za Saudia, Imarati, Misri na Bahrain ziache ndoto za alinacha na njozi zisizoagulika.

Shirika la habari la Mehr limemnukuu Muhammad bin Abdul Rahman Aal Thani akisema hayo na kuongeza kuwa, mwamko, mshikamano na umoja wa wananchi wa Qatar mbele ya njama zinazoikabili nchi yao ni jambo la kupigiwa mfano. Aidha amewataka viongozi wa nchi nne zilizoiwekea vikwazo Doha kushughulishwa na matatizo ya nchi zao badala ya kujishughulisha na masuala ya Qatar.

Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia (kushoto) na Amir wa Qatar, Tamim bin Hamad Aal Thani

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar pia amesema, nchi marafiki wa Doha zinafanya juhudi kubwa za kupunguza wasiwasi uliozushwa na nchi hizo nne za Kiarabu dhidi ya Qatar lakini kuna baadhi ya nchi katika eneo hili zinafanya njama za kuzusha mgogoro mpya.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Saudi Arabia ilitishia kuishambulia kijeshi Qatar iwapo itanunua mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya makombora wa S400 kutoka kwa Russia. Harakati ya Answarullah ya Yemen iliitoa wasiwasi Qatar kwa kuiambia kuwa isishughulishwe na vitisho hivyo hewa vya Saudi Arabia kwani ukoo wa Aal Saud na Imarati wamekwama kwenye kinamasi nchini Yemen.

Nayo Russia ilijibu vitisho hivyo vya Saudi Arabia kwa kuitahadharisha isifikirie kabisa kuishambulia kijeshi Qatar kwa sababu ya kununua mfumo huo wa kujilinda na makombora.

Ngao ya makombora ya S400

 

Naibu mkuu wa kamati ya ulinzi na usalama katika bunge la Russia Alexei Kondratiev alisema kuwa msimamo wa Saudia wa kutishia kuishambulia Qatar kwa kuununua ngao ya makombora ya S400 hautokwamisha uzalishaji wa makombora hayo ya anga kwa ajili ya serikali ya Doha.

Aidha Alexei Kondratiev ambaye pia ni seneta nchini Russia alisema, matamshi ya vitisho ya Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia kwamba nchi yake imejiandaa kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Qatar iwapo itanunua ngao ya makombora wa S400, yanadhibihirisha kiasi cha hali ya juu cha chokochoko iliyo nayo Saudi Arabia. Ameongea kwamba, ni jambo lililo wazi kwamba hivi sasa Riyadh inajaribu kulidhibiti eneo la Mashariki ya Kati kwa kutumia mabavu na kwamba hatua ya serikali ya Doha ya kuimarisha uwezo wake wa kijeshi kupitia ngao ya makombora ya S400 ya Russia itaongeza nguvu za kijeshi za Qatar na kwa ajili hiyo ndio maana Saudi Arabia imeingiwa na wahka. 

Tags