Mamia ya askari wa Marekani wanaoondolewa Syria kupelekwa Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56736-mamia_ya_askari_wa_marekani_wanaoondolewa_syria_kupelekwa_iraq
Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema mamia ya wanajeshi wa nchi hiyo wanaoondolewa Syria watapelekwa nchini Iraq.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 20, 2019 07:30 UTC
  • Mamia ya askari wa Marekani wanaoondolewa Syria kupelekwa Iraq

Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema mamia ya wanajeshi wa nchi hiyo wanaoondolewa Syria watapelekwa nchini Iraq.

Mark Esper amedai kuwa amefanya mazungumzo na mwenzake wa Iraq juu ya kupelekwa magharibi mwa nchi hiyo ya Kiarabu wanajeshi 700 wa Marekani watakaoondolewa Syria.

Rais Donald Trump aliagiza kuondoka nchini Syria wanajeshi elfu moja wa Marekani, baada ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kumuambia katika mazungumzo ya simu kuwa nchi yake inataka kuanzisha operesheni ya kukabiliana na kuwarejesha nyuma wanamgambo wa Kikurdi kaskazini mwa Syria.

Wiki iliyopita Uturuki ilianzisha hujuma hizo dhidi ya Syria ambapo Rais Erdogan amesema lengo la mashambulizi hayo ni kuangamiza kundi la PKK la eneo la Kurdistan la Uturuki, kundi la Wakurdi wa Syria na pia kundi la kigaidi la Daesh (ISIS). 

Vikosi vya jeshi la Uturuki nchini Syria

Uturuki imetekeleza mashambulizi hayo dhidi ya Syria pamoja na kuwa operesheni hiyo imepingwa vikali kieneo na kimataifa. 

Hata hivyo kwa sasa wanajeshi wa Uturuki wamesitisha operesheni zao za kijeshi kaskazini mwa Syria kwa muda wa siku tano ili kuwapa fursa wanamgambo wa Kikurdi warudi nyuma umbali wa maili 20 ndani ya ardhi ya Syria kutoka mpaka wa nchi hiyo na Uturuki; baada ya Rais Erdogan kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence.