Qatar imefanikiwa kukabiliana na vikwazo vya Saudia na waitifaki wake
(last modified Wed, 06 Nov 2019 07:44:00 GMT )
Nov 06, 2019 07:44 UTC
  • Qatar imefanikiwa kukabiliana na vikwazo vya Saudia na waitifaki wake

Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani amesema nchi yake imefanikiwa katika kukabiliana na vikwazo vya Saudi Arabia na waitifaki wake.

Akihutubu Jumanne katika Baraza la Shura, ambalo humshauri Emir wa Qatar kuhusu miswada ya sheria, Sheikh Tamim amesema Qatar imefanikiwa kukabiliana na taathira hasi za vikwazo na imeweza kufikia malengo yake ya juu ya kiuchumi.

Tangu tarehe 5 Juni mwaka 2017, Saudi Arabia, Imarati (UAE), Bahrain na Misri zilivunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa sababu ya misimamo ya Doha ambayo haiwiyani na sera za utawala wa Riyadh. Mbali na kuiwekea vikwazo, nchi hizo nne zimeifungia Qatar pia mipaka yao ya nchi kavu, baharini na angani.

Mzingiro huo uliwekwa baada ya Saudia na waitifaki wake kuituhumu Qatar kuwa 'inaunga mkono ugaidi' madai ambayo Qatar imeyakanusha vikali. Saudia na waitifaki wake wameiwekea Qatar masharti kadhaa ya kuondolewa vikwazo na mzingiro ikiwa ni pamoja na kukata uhusiano na Iran na kufunga kituo cha kijeshi cha Uturuki nchini Qatar. Serikali ya Qatar imesema haitatekeleza masharti hayo na kusema ina uhuru wa kufuata sera inazotaka.

 

Tags