Qatar: Hatuwezi kuzisahau nchi zilizotusaidia katika kipindi cha vikwazo
(last modified Tue, 17 Dec 2019 03:10:10 GMT )
Dec 17, 2019 03:10 UTC
  • Qatar: Hatuwezi kuzisahau nchi zilizotusaidia katika kipindi cha vikwazo

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar amesema kuwa, licha ya Doha kuyafanyia uchunguzi matakwa ya nchi za Ghuba ya Uajemi yenye lengo la kutatua mozozo na hitilafu, lakini katu haitazisahau nchi zilizoisaidia Qatar katika kipindi cha vikwazo na mashinikizo.

Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali yay televisheni ya CNN na kuongeza kwamba, mkwamo wa kuanza mazungumzo na Saudi Arabia umeondolewa.

Alipoulizwa kama utatuzi wa hitilafu hizo utachuukuua muuda gani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar amesema kuwa, kwa sasa mazungumzo yangali katika hatua za awali na kunahitajika kupita muda kidogo ili kupatikana tena hali ya kuamianiana. 

Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amesema kuwa, kwa sasa Doha ingali inayayafanyia tathmini masharti ya nchi za Ghuba ya Uajemi. 

Itakumbukwa kuwa tarehe 5 Juni 2017, Saudia iliongoza nchi nyingine za Kiarabu za Misri, Imarati na Bahrain kuiwekea vikwazo vya angani, baharini na ardhini nchi ndogo ya Qatar na kukata kabisa uhusiano wao na Doha. 

Image Caption

 

Mnamo tarehe 23 Juni, nchi hizo nne ziliipatia Qatar orodha ya masharti 13 na kutangaza kuwa kurejeshwa tena uhusiano wa kawaida na nchi hiyo kutategemea utekelezwaji wa masharti yote hayo na serikali ya Doha.

Masharti muhimu zaidi ambayo Saudi na washirika wake wameishurutisha Qatar ni kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran na Hizbullah ya Lebanon, kuifunga stesheni ya televisheni ya Aljazeera na kuondoa kituo cha kijeshi cha Uturuki ndani ya ardhi ya Qatar. Serikali ya Doha imeyakataa masharti hayo..

Tags