Saudia yaongoza duniani kwa ufanyaji israfu kubwa katika chakula
Saudi Arabia inaongoza kati ya nchi 25 duniani zinazomwaga na kutupa jaani kiwango kikubwa zaidi cha chakula.
Kitengo cha wanataaluma wa masuala ya biashara cha jarida la The Economist, kimetangaza kuwa, kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi uliofanywa, nchi 25 zinamiliki karibu asilimia 87 ya Jumla ya Pato la Dunia na kwamba Wasaudia wanaongoza kati ya raia wa nchi zote duniani katika israfu ya umwagaji na utupaji mabaki ya chakula.
Wakati Wizara ya Mazingira, Maji na Kilimo ya Saudia imetangaza kuwa kila raia mmoja wa nchi hiyo humwaga kilogramu 250 za chakula kwa mwaka, kulinganisha na wastani wa dunia wa kilo 115, Kitengo cha Wanataaluma cha The Economist kinasisitiza kuwa, kiwango halisi cha utupaji chakula unaofanywa na kila raia mmoja wa nchi hiyo ni kikubwa zaidi ya kiwango hicho rasmi kilichotangazwa na serikali ya Riyadh. Kwa mujibu wa kitengo hicho, kiwango hicho ni karibu kilo 427 za chakula kwa mwaka.

Imeelezwa kuwa israfu hiyo ya umwagaji na utupaji chakula, mbali na kuisababishia Saudia hasara ya kiuchumi ya mabilioni ya dola kwa mwaka, inasababisha pia uharibifu wa mazingira na madhara ya kijamii. Aidha imeelezwa kwamba, umwagaji chakula mikahawani, katika sherehe na matukio ya kijamii ni mkubwa nchini Saudi Arabia kwa sababu ya ada na mazoea ya utoaji chakula kwa kiwango kikubwa zaidi ya kinachohitajika kwa kutumia jina la ukarimu.
Wakati nchi kadhaa za Kiarabu zinaongoza kwa israfu ya chakula, kwa mwaka wa tano sasa, wananchi wa nchi masikini zaidi ya Kiarabu ya Yemen wanaandamwa na hujuma na mashambulio ya kijeshi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia, ambayo mbali na kuteketeza roho za watu, yameisababishia nchi hiyo baa kubwa zaidi la njaa duniani.
Wakati huohuo, watu wapatao bilioni moja wanateseka kwa baa la njaa na lishe duni katika maeneo mbali mbali duniani.../