Mahathir: "Muamala wa Karne" ni mpango wa kibaguzi unaohalalisha uvamizi
Waziri Mkuu wa Malaysia amesema kuwa mpango wa Mumala wa Karne uliobuniwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili eti ya amani ya Mashariki ya Kati umetayarishwa na dhalimu na mchokozi, si wa kiadilifu na utapelekea kujitokeza hali ya ubaguzi wa kizazi (Apartheid).
Mahathir bin Mohamad ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa tatu wa Bunge la Malaysia kuhusu Quds tukufu ametoa wito wa kutekelezwa maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya Wapalestina ya kujiamulia mambo yao wenyewe. Vilevile ameitahadharisha jamii ya kimataifa kuhusu mauaji ya kizazi yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina.
Waziri Mkuu wa Malaysia amesema kuwa, mpango wa Muamala wa Karne uliotayarishwa na serikali ya Trump kwa kushirikiana na Israel hauna ufumbuzi wa aina yoyote juu ya suala la kuundwa dola huru la Palestina. Amesema Malaysia inautambua mpango huo kuwa haukubaliki na ni wa kidhalimu kupita kiasi.
Jumanne ya tarehe 28 Januari, Rais wa Marekani, Donald Trump alizindua mpango wa Muamala wa Karne akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu.
Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, Quds Tukufu itakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni, wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki ya kurejea katika ardhi za mababu zao na Palestina itamiliki tu ardhi zitakazosalia huko katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.
Mpango huo umepingwa vikali na jamii ya kimataifa na hata ndani ya Marekani kwenyewe.
Wajumbe 107 wa chama cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani wamemwandikia barua rais wa nchi hiyo Donald Trump wakiupinga vikali mpango huo.