Waziri Mkuu wa Palestina: Muamala wa Karne utazikwa hivi karibuni
-
Mohammad Shtayyeh
Waziri Mkuu wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameuambia Mkutano wa Usalama wa Munich kwamba mpango wa Kimarekani wa Muamala wa Karne utazikwa kaburini hivi karibuni.
Mohammad Shtayyeh amelaani mpango huo uliopendekezwa na Rais Donald Trump wa Marekani na kusema: Muamala wa Karne si lolote ghairi ya hati ya maelewano baina ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais Donald Trump wa Marekani.
Itakumbukwa kuwa tarehe 28 mwezi uliopita wa Januari Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu walizindua mpango eti wa amani wa Muamala wa Karne katika ikulu ya White House.
Mpango huo mpya wa serikali ya Marekani unaolenga kukanyaga kikamilifu haki za taifa la Palestina umebuniwa kwa kushirikiana na nchi kadhaa vibaraka za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia.
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa, matamshi yaliyotolewa na Waziri Mshauri katika Masuala ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al Jubeir akisifu mpango wa Muamala wa Karne ni kielelezo cha ushirikiano uliopo baina ya Riyadh na Washington kwa ajili ya kutokomeza kabisa kadhia ya Palestina.
Alkhamisi iliyopita Waziri Mshauri katika Masuala ya Nje wa Saudia, Adel al Jubeir alidai kuwa, mpango wa Muamala wa Karne uliopendekezwa na Donald Trump una vipengee chanya na unaweza kutumiwa kama msingi wa kuanza mazungumzo.
Msemaji wa harakati ya Hamas amesema matamshi kama haya yanausaidia utawala wa Kizayuni wa Israel na serikali ya Marekani katika kupeleka mbele zaidi mpango huo wa Muamala wa Karne unaokanyaga haki za taifa la Palestina.
Kuitambua rasmi Baitul Muqaddas (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, kuupatia utawala huo haramu umiliki wa asilimi 30 ya eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, kupingwa haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea nchini kwao na kupokonywa silaha kikamilifu itakayoitwa nchi ya Palestina ni miongoni mwa vipengele vya mpango huo wa udhalilishaji.