Aal Saud na corona ya kisiasa
(last modified Tue, 24 Mar 2020 02:34:56 GMT )
Mar 24, 2020 02:34 UTC
  • Aal Saud na corona ya kisiasa

Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazoutumia kisiasa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na kirusi cha corona.

Maradhi yanayosababishwa na kirusi cha corona hayajaikumba nchi makhsusi, bali ni janga lililoenea ulimwengu mzima, kiasi kwamba hivi sasa zaidi ya nchi 190 zimeshakumbwa na kirusi hicho hatari na angamizi. Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa hivi karibuni na serikali ya Saudi Arabia, hivi sasa kuna watu 511 nchini humo walioambukizwa kirusi cha corona. Lakini katika kipindi cha mwezi mmoja sasa, badala ya utawala wa Saudia kuchukua hatua za kuuzuia na kuudhibiti ugonjwa wa covid-19, umekuwa ukitumia kila mbinu kunufaika nao kisiasa.

Saudia imesitisha ibada ya Umra kwa kuhofia maambukizo ya kirusi cha corona

Katika hatua ya kwanza, utawala wa Aal Saud uliituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ndio iliyosambaza kirusi hicho katika eneo la Asia Magharibi. Halmashauri ya Mawaziri wa Saudi Arabia ilidai kwamba, hatua zinazochukuliwa na Iran zinakwamisha juhudi zinazofanywa kimataifa kupambana na corona, hivyo Iran inabeba dhima ya moja kwa moja ya kueneza maradhi ya covid-19. Halmashauri hiyo ilidai kuwa, Iran iliwaruhusu raia wa Saudia waingie katika ardhi yake bila kuzipiga muhuri pasi zao za kusafiria na kwamba watu hao waliorejea Saudia ndio walioingiza virusi vya corona nchini humo. Madai hayo ya utawala wa Aal Saud ni muendelezo wa vita vya niaba ulivyoanzisha kupambana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu mwaka 2011 hadi sasa. Tuhuma hizo zilitolewa ilhali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilishaziomba mara kadhaa nchi waitifaki wa Saudia ikiwemo Bahrain ichukue hatua ya kuwarejesha nchini humo raia wake walioko Iran, lakini utawala wa Aal Khalifa haukujali wala kuthamini maisha ya raia zake.

Igizo la pili la corona ya kisiasa ambalo limeigizwa ndani ya Saudi Arabia ni muamala wa utawala wa Aal Saud kwa raia wa Kishia wa nchi hiyo. Wakati ugonjwa wa corona umesambaa katika miji mingi ya Saudia, hatua ya mwanzo aliyochukua Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ilikuwa ni kuliwekea karantini eneo la Waislamu wa Kishia tu la Qatif. Madai uliyotoa utawala wa Aal Saud ni kwamba, raia kadhaa wa Saudia kutoka eneo hilo wamekuwa wakifanya safari za kuja na kurudi hapa nchini Iran. Madai hayo yalitolewa, ilhali raia wengi wa Saudi Arabia wamekuwa wakisafiri zaidi kuelekea nchi za mashariki ya Asia na hasa China, kuliko hata Iran. Ukweli ni kwamba, utawala wa Saudia umeutumia ugonjwa wa corona kuendeleza mwenendo wake wa kuwakandamiza raia katika eneo la Qatif, ambalo wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Jamaa wa Wapalestina waliofungwa jela Saudia wakiutaka utawala wa Aal Saud uwaachie huru watu wao

Na igizo la tatu la corona ya kisiasa lililoigizwa ndani ya Saudia linahusu wafungwa Wapalestina. Hivi sasa kuna Wapalestina zaidi ya 60 wanaoshikiliwa kwenye jela za Saudi Arabia kwa tuhuma za kuwa na mahusiano na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na ambao wanaishi katika hali na mazingira yasiyoridhisha. Wafungwa hao Wapalestina wananyimwa haki ya kuwasiliana na mawakili wao au hata kukutana na jamaa wa familia zao, ambapo hivi karibuni maafisa wa utawala wa Aal Saud wamepunguza hata muda wa mazungumzo ya simu ya wafungwa. Kwa sababu hiyo Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameikosoa Riyadh na kueleza kwamba, kuachiwa huru wafungwa Wapalestina walioko Saudia ni suala lenye udharura kiutu na kitaifa, hasa kutokana na maambukizi ya kirusi cha corona yanayohatarisha maisha ya wafungwa hao. Familia za Wapalestina waliofungwa jela nchini Saudi Arabia, nazo pia zinataka jamaa zao hao waachiliwe huru, zikisisitiza kwamba, utawala wa Aal Saud umetumia mashtaka bandia kuwafungulia kesi na kuwafunga jela watu hao. Ukweli ni kwamba, utawala wa Aal Saud, ambao una mikinzano mingi na Hamas kiutambulisho na kimsimamo unaitumia kadhia ya corona kuendeleza mbinyo na ukandamizaji dhidi ya wafungwa wa Kipalestina unaowashikilia…/