Yemen yasisitiza kuendelea kujibu mapigo kwa hujuma na mashambulio ya Saudia
Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen amesisitiza kuwa vyombo vya kijeshi na vya utawala vya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia vitaendelea kushambuliwa madamu muungano huo vamizi ungali unaendeleza uchokozi na mzingiro dhidi ya Yemen.
Brigedia Jenerali Yahya Saree ameashiria jinai zinazofanywa na muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen na kusisitiza kwamba: Jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen vitaendelea kutumia haki yao ya kisheria ya kuwalinda watu wao na nchi yao.
Saree amesema, uwezo na nguvu za kujihami ilizonazo Yemen leo hii ni kubwa zaidi kulinganisha na huko nyuma na akaongeza kwamba: Jeshi na vikosi vya Yemen havijatumia uwezo wake wote hadi sasa hivyo adui inapasa alielewe hilo na kuacha uchokozi na mzingiro wake dhidi ya Yemen.
Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen amesema pia kuwa: Wananchi wa Saudi Arabia ambao wanadhulumiwa na utawala wa Aal Saud hawatoshambuliwa na jeshi la Yemen, na kwamba mashambulio ya jeshi hilo yataendelezwa dhidi ya taasisi za kijeshi na za utawala wa Saudia zilizo mstari wa mbele katika hujuma na mashambulio dhidi ya wananchi wa Yemen.
Katika siku za karibuni muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia umefanya mashambulio makali ya anga mara kadhaa dhidi ya vituo vikuu na muhimu vya Yemen katika mji mkuu Sana'a na maeneo mengine ya nchi hiyo.../