Sababu za umuhimu wa safari ya Biden kwa Saudi Arabia
Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kuanza safari yake Asia Magharibi leo Julai 13 na safari hiyo inatazamiwa kumalizikia Saudia mnamo Julai 16.
Katika mwaka mmoja na nusu uliopita, uhusiano kati ya Washington na Riyadh umeonekana kuwa na mabadiliko makubwa ikilinganishwa na hapo awali. Saudi Arabia, ambayo ilifurahia uhuru mpana wa kufanya itakalo katika sera zake za ndani na nje katika kipindi cha Donald Trump, imekabiliwa na ukosoaji wa wazi wakati wa urais wa Biden.
Nukta kuu za ukosoaji zimehusiana na masuala ya haki za binadamu kutokana na ukiukaji mkubwa na ulioenea wa haki za binadamu unaofanywa na Saudi Arabia na kuhusika mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Mohammed bin Salman katika jinai hizo. Pamoja na hayo, mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022, msimamo wa Biden kuhusu Saudi Arabia na hata Bin Salman umebadilika hatua kwa hatua, na hakuna tena ukosoaji mkali ulioonekana hapo awali katika uwanja huo. Vita vya Russia dhidi ya Ukraine ndio sababu kuu ya Biden kubadili msimamo kuhusu Riyadh. Vita vya Ukraine vimesababisha kuongezeka pakubwa bei ya mafuta duniani.
Hadi sasa Saudi Arabia imepinga matakwa ya nchi za Magharibi ya kutaka kuongeza uzalishaji wa mafuta ghafi ya petroli dunaini, lakini mabadiliko ya misimamo ya Biden yanaonyesha kuwa Riyadh kwa mara nyingine tena imeweza kutumia mafuta kama wenzo wa kufikia malengo yake katika sera za kigeni, hasa kuhusiana na Marekani. Hata kama utawala wa Biden unasisitiza kuwa mafuta sio ajenda kuu ya safari yake, kwa kusema mnamo Juni 12: "Safari hii inahusu masuala makubwa zaidi", mafuta yanaonekana kuwa sababu kuu ya ziara ya Biden nchini Saudi Arabia.
La muhimu ni kwamba ziara ya rais wa Marekani nchini Saudi Arabia ni muhimu sana kwa kwa nchi hiyo ya kifalme. Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, anahitaji uungwaji mkono wa Washington ili kuketi kwenye kiti cha ufalme wa nchi hiyo. Kimsingi, kufikia kilele cha madaraka na kuendelea kuwepo watawala walioko madarakani katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kunahitaji uungaji mkono wa serikali ya Marekani. Kwa sababu hiyo, Bin Salman, ambaye hakuwa mbali na kiti cha ufalme cha Saudi Arabia wakati wa enzi ya Trump, aliona nafasi yake iko hatarini baada ya Biden kuingia madarakani, kwa sababu utawala wa Biden ulikuwa na ajenda ya kuwaunga mkono wapinzani wa Bin Salman. Kwa hiyo, safari ya Biden nchini Saudia na kukutana kwake na Mohammed bin Salman yamkini kukaashiria mwisho wa shinikizo dhidi ya Mwana wa Mfalme huyo wa Saudia ambaye ni maarufu kwa lakabu ya MBS.
Nukta nyingine muhimu ni kwamba, ziara ya Biden nchini Saudi Arabia licha ya ukosoaji mkubwa aliokuwa nao hapo kabla kwa ufalme huo, inaonesha kuwa, Riyadh ina nafasi muhimu katika matukio ya Asia Magharibi na pia katika siasa za nje za madola makubwa. Hivyo Saudia inataka kutumia safari ya Joe Biden kufikia malengo yake ya kujitanua katika eneo.

Kuhusiana na hilo, Dalia Dassa Kaye aliandika katika uchambuzi uliochapishwa katika jarida la Foreign Policy kuwa, "Wakati Rais wa Marekani Joe Biden alipoanza urais wake, alibadilisha muelekeo wa rais wa awali, Trump, katika muamala wa karibu na madikteta kama vile Mohammed bin Salman, ambaye anachukuliwa kuwa kiongozi halisi wa Saudi Arabia na alionekana kuwa mkali kwa watawala kama hao. Hata hivyo, baada ya mwaka mmoja Biden ameamua kutembelea Saudi Arabia katika safari yake ya kwanza ya Asia Magharibi katika urais wake. Uamuzi huo umewakatisha tamaa wale waliodhani kuwa Biden ni bingwa wa haki za binadamu. Kumzawadia Mohammed bin Salman kwa kupeana mkono naye na kupiga picha katika kasri ya mwanamfalme huyo ni kukiri kwamba watawala wa kiimla wanaweza kuwaua wapinzani wao almradi tu watoe dhamana kwamba mafuta yatanedelea kuuzwa katika masoko ya kimataifa."
Nukta ya mwisho ni kwamba iwapo safari ya Biden nchini Saudi Arabia haitafanikisha malengo yake hasa katika uwanja wa nishati, huko kutahesabiwa kuwa ni kushindwa kwingine muhimu katika uga wa sera zake za kigeni.