Kuendelea Marekani kulitumia vibaya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Serkali ya China imepinga ombi la Marekani na baadhi ya waitifaki wake la kuitishwa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Korea Kaskazini.
Ofisi ya mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa sambamba na kupinga kuitishwa kikao cha Baraza la Usalama kuhusu masuala ya haki za binadamu huko Korea Kaskazini imesema kuwa, kikao hicho kitazidi tu kuifanya hali kuwa mbaya na hakitotatua jambo lolote.
Ofisi hiyo ya mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa. vile vile imesema, kwa mtazamo wa Beijing, kuitishwa kikao kama hicho hakuna faida yoyote kwa Baraza la Usalama ndio maana inapinga. Kwani jukumu la Baraza la Usalama ni kulinda usalama na amani kimataifa na si masuala ya haki binadamu. Ofisi hiyo ya kudumu ya China katika Umoja wa Mataifa imesema kuwa, kikao cha Baraza la Usalama cha kuzungumzia haki za binadamu Korea Kaskazini ni kitu kilichoko nje ya majukumu ya baraza hilo na kwamba masuala ya haki za binadamu yataingilia masuala ya kisiasa na kuzidisha tu mivutano.
Nchi za Marekani, Albania na Japan zimetaka kufanyike kikao cha Baraza la Usalama kuzungumzia haki za binadamu Korea Kaskazini. Vyombo vya habari vya Magharibi vimewanukuu viongozi wa Marekani wakidai kuwa wana uhakika wa kupata kwa uchache kura 9 za kuidhinisha kuitishwa kikao hicho.
Siku moja kabla ya Marekani kuzusha suala la kujadiliwa haki za binadamu huko Korea Kaskazini ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Kim Jong-un, kiongozi wa Korea Kaskazini wakati alipokuwa anakagua kiwanda cha kuzalisha silaha za kivita alitoa dkrii ya kuzidishwa uzalishaji wa makombora ya kukabiliana na ubeberu wa madola ya Marekani na chokochoko za Korea Kusini. Inavyoonekana ni kwamba serikali ya Marekani imeamua kuchukua hatua zozote zile kuhakikisha kuwa inavuruga miradi ya makombora ya Korea Kaskazini. Uhakika huu nao ni lazima tuuzingatie kwamba Marekani inazitumia vibaya taasisi za kimataifa kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa manufaa yake binafsi bila ya kujali manufaa ya kitaifa ya nchi nyingine.
Kwa kweli, moja ya matatizo makubwa yanayoitesa dunia leo, ni kuchukuliwa hatua za upande mmoja za Marekani dhidi ya nchi nyingine duniani. Wakati huo huo kufuata kibubusa nchi kama Japan; siasa za Marekani, kunazidi kulipandisha kiburi dola hilo la kibeberu. Kabla ya hapo wanasiasa walioko madarakani hivi sasa huko Japan wamekuwa wakichukua misimamo ya kujidunisha na kujidhalilisha mbele ya Marekani licha ya kwamba Japan ni nchi kongwe yenye historia na ustaarabu mkubwa kuliko Marekani.
Wakati huo huo Fuad Izadi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tehran na mtaalamu wa masuala ya Marekani anasema, kila nchi ambayo ina angalau kiwango kidogo tu cha uhuru katika siasa zake za nje, basi inapaswa kuchukua hatua kama ya China ya kupinga kuitishwa kikao cha Baraza la Usalama kwa manufaa ya dola la kibeberu la Marekani.
Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba viongozi walioko madarakani hivi sasa huko Marekani, wameamua kutumia kila wawezalo kufanikisha malengo yao haramu. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa bali hata Umoja wa Ulaya ni miongni mwa taasisi za kimataifa ambazo daima zinatumiwa vibaya na viongozi wa Marekani kwa ajili ya kukandamiza mataifa mengine na kudhamini maslahi yao haramu ya kiistikbari.
Kiujumla tunapaswa kusema kuwa, viongozi wa Marekani wanafanya njama za kuzishinika nchi kama China kupitia kuishinikiza Korea Kaskazini. Lengo la viongozi wa Marekani ni kuonesha kuwa China imetengwa kimataifa. Lakini inavyoonekana ni kuwa viongozi wa China wanazidi kuimarisha nguvu zao kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Washington duniani, suala ambalo limewatia hofu sana viongozi wa dola la kibeberu la Marekani.