Takwa la China kwa Marekani la kusitisha kuiuzia silaha Taiwan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i101554-takwa_la_china_kwa_marekani_la_kusitisha_kuiuzia_silaha_taiwan
Licha ya kuwa China imeitaka Marekani mara kadhaa iache kuiuzia silaha na zana za kijeshi Taiwan, lakini Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon imetangaza kwa ujeuri kabisa kwamba, itaipatia Taiwan silaha mpya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 28, 2023 00:21 UTC
  • Takwa la China kwa Marekani la kusitisha kuiuzia silaha Taiwan

Licha ya kuwa China imeitaka Marekani mara kadhaa iache kuiuzia silaha na zana za kijeshi Taiwan, lakini Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon imetangaza kwa ujeuri kabisa kwamba, itaipatia Taiwan silaha mpya.

Pentagon imetangaza kuwa serikali ya Marekani imeidhinisha uuzaji wa mifumo ya utafutaji na ufuatiliaji kwa ajili ya ndege za kijeshi za F-16 pamoja na vifaa vingine vya kijeshi kwa Taiwan. Hii ina maana kwamba, serikali ya Marekani inafuata sera ya kuendeleza ushirikiano wa kijeshi na Taiwan ili kuishinikiza zaidi China. Kwa kuzingatia kwamba Taiwan haina ubavu wa kukabiliana kijeshi na China, swali muhimu linalojitokeza ni kuwa, nini malengo ya mkataba wa silaha kati ya Taiwan na Marekani? Weledi wa masuala ya kisiasa wanaashiria  mambo kadhaa kuhusiana na malengo ya Marekani.

Kwanza, Marekani inaiona Taiwan kama soko la silaha lenye faida lukuki. Pili, Marekani inaifanya Taiwan kama wenzo wake wa mashinikizo dhidi ya China. Nukta ya tatu ni kuwa, Marekani inafuatilia kuchochea ushindani wa silaha katika Lango Bahari la Taiwan na Asia ya Mashariki.

Li Shu Zhang, mchambuzi wa masuala ya kimataifa anasema kuhusiana na hili kwamba: "Marekani inadhani kwamba kupitia Taiwan sambamba na kuishinikiza China itaweza kuitishwa Beijing matakwa yake.

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Marekani inafahamu vyema mstari mwekundu wa China katika masuala ya ardhi na mamlaka ya kujitawala Taiwan na imesisitiza hilo mara chungu nzima. Hata hivyo, pamoja na kuiuzia Taiwan zana za hali ya juu za kijeshi, Washhington imeongeza pia uungaji mkono wake kwa wanaharakati wa kupigania kujitenga wa eneo hilo, jambo ambalo limekabiliwa na upinzani na maandamano ya kulalamikia hilo.

 

Taiwan nayo kwa upande wake kwa kununua silaha na zana za kijeshi inafuatilia malengo kadhaa. Lengo la kwanza ni kuiridhisha Marekani ili iendelee kuiunga mkono mkabala wa China. Kwani kununua silaha za gharama kubwa kutoka Marekani, kimsingi ni kuwaridhisha wamilikki wa makampuni ya uundaji na uzalishaji silaha nchini Marekani. Sambamba na kununua silaha Taiwan inatumia gharama kubwa kukarabati na kuhifadhhi silaha hizo.

Lengo la pili la kisiwa la Taiwan la kununua silaha ni kutanua misuli mbele ya China, huku lengo la tatu likiwa ni kuwa, kwa kununua silaha Taiwan inataka kuonyesha kuwa, China ni tishio na kwa hatua hiyo inakusudia kujionyesha mbele ya macho ya walimwengu kwamba, inadhulumiwa. Kwa muktadha huo na kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon, kifurushi kipya cha silaha kinakachopatiwa Taiwan kina thamani ya dola milioni 500.

Imedaiwa katika taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani kwamba, uuzaji wa zana hizo hautabadilisha mlingano wa kijeshi katika eneo la Asia Mashariki na kwamba, ni shehena mpya ya silaha inayosaidia tu maslahi ya kitaifa, kiuchumi na kiusalama ya Marekani kwa kusaidia kuboresha vikosi vya kijeshi na kudumisha uwezo wa ulinzi wa Taiwan. Hata hivyo, hii kwamba, Taiwan itaweza vipi kusaidia kudhamini usalama wa Marekani dhidi ya uwezekano wa mashambulio ya Uchina na Russia na hata Korea Kaskazini, ni jambo linalotia shaka madai yote yaliyotolewa na Marekani kuhusu uuzaji wa silaha kwa Taiwan.

Henry Kissinger, mchambuzi mwandamizi wa kisiasa wa Marekani

 

Pamoja na hayo, Henry Kissinger, mchambuzi mwandamizi wa kisiasa wa Marekani, ameonya mara kadhaa Washington kuhusu madhara ya kuvuka mstari mwekundu wa China hasa kwa kuzingatia kwamba, China haiko tayari kulegeza kamba kuhusiana na Taiwan na majibu ya Beijing kkwa chokochoko za Washington yanaweza kuwa na matokeo yasiyoweza kufidika.

Hata hivyo, Pentagon imesisitiza kwamba mauzo ya silaha yataboresha uwezo wa Taiwan kukabiliana na vitisho vya sasa na vya siku zijazo kwa kusaidia kuboresha uwezo wa Taiwan wa kulinda anga yake na kuhakikisha usalama wa kikanda.

Hii ni katika hali ambayo, uwezo wa kijeshi wa Taiwani kadiri utakavyoongezeka kwa kiwango chochote kile, haitakuwa na ubavu wa kukabiliana na nguvu za kijeshi za China, na wakati huo huo, ni jambo lililo mbali kwa Marekani kuingia vitani na kuihami Taiwani endapo kutaibuka vita baina ya pande mbili.

China inakichukulia kisiwa cha Taiwan kuwa sehemu ya ardhi yake na inaziona safari za maafisa wa Taiwan nchini Marekani au kuwepo kwa maafisa wa nchi za Magharibi katika kisiwa hicho kuwa ni ukiukaji wa kanuni ya "China moja". Kwa hivyo, Beijing tayari imesisitiza kwamba ikiwa italazimu, itatumia vikosi vya kijeshi kukiunganisha kisiwa hiki. Ujumbe ambao unaweza kuwa kizuizi dhidi ya ushiriki wowote wa Marekani katika uwezekano wa vita katika Lango Bahari la Taiwan. Serikali ya Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China na kwamba chaguo la kutumia nguvu za kijeshi ili kushika hatamu za udhibiti wa kisiwa hicho bado lipo mezani.