BRICS na miungano mipya katika ngazi ya mfumo wa kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i101668-brics_na_miungano_mipya_katika_ngazi_ya_mfumo_wa_kimataifa
Baada ya nchi 6 mpya kujiunga na kundi la BRICS, sasa kundi hili lenye nchi 11 wanachama limeunda kambi mpya katika ngazi ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2023 22:58 UTC
  • BRICS na miungano mipya katika ngazi ya mfumo wa kimataifa

Baada ya nchi 6 mpya kujiunga na kundi la BRICS, sasa kundi hili lenye nchi 11 wanachama limeunda kambi mpya katika ngazi ya kimataifa.

Mkutano wa 15 wa kilele wa BRICS ulifanyika wiki iliyopita katika wilaya ya masuala ya fedha ya Sandton mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini. Katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na viongozi wa China, Brazil, India na mwakilishi wa Russia, Rais wa Afrika Kusini alitangaza kuwa kundi la BRICS limekubali kuzipa uanachama nchi za Iran, Argentina, Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Ethiopia. Wanachama 6 wapya watajiunga rasmi na kundi hilo mwanzoni mwa ujao wa 2024. Baada ya tukio hilo, kumetolewa uchambuzi mbalimbali kuhusu nafasi ya BRICS katika ngazi ya kimataifa.

Miongoni mwa uchambuzi huo ni kwamba, kwa kujiunga nchi 6 mpya, ambazo kila moja ina umuhimu mkubwa wa kiuchumi na kisiasa, kundi la BRICS linaweza kuunda kambi mpya katika kiwango cha mfumo wa kimataifa. Sababu kuu ya mtazamo huo ni kwamba, wanachama wa zamani na wapya wa BRICS wanadhibiti sehemu kubwa ya uchumi wa dunia, na kwa upande mwingine wanachama hao wanapinga mfumo wa kisiasa wa kambi moja.  

BRICS

Salem Nasser, mtaalam wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha FGV Direito SP cha Brazili, anasema, maombi ya kujiunga na BRICS yanaonyesha kuwa kuna mabadiliko katika uwiano wa nguvu katika uwanja wa kimataifa. Nasser anasema: BRICS ni kambi mpya ya nguvu ya kiuchumi na kisiasa ambayo itashindana na udhibiti wa Amerika Kaskazini.

Mehmet Ali Guller, mchambuzi wa Kituruki, pia anaamini kuwa, BRICS ni moja ya nguzo muhimu zaidi za mfumo mpya wa ulimwengu na imetoa pigo kubwa kwa vita vya kuwania nguvu za kisiasa na kinishati vya Marekani.

Suala jingine ni kwamba, wanachama wa zamani na wapya wa BRICS, wanaweza kufanya maamuzi muhimu katika uwanja wa uchumi katika ngazi ya kimataifa. Ushawishi huu utakuwa mkubwa hasa katika sekta ya nishati, kwa sababu Saudi Arabia, Russia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na UAE ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani. Ushirikiano wa nchi hizi katika nyanja za nishati unaweza kuwa na athari nyingi mbaya kwa nchi za Magharibi na kuathiri uchumi wa dunia. Vilevile upanuzi wa BRICS utaongeza mauzo ya nje ya kundi hili kimataifa kutoka 20.2% hadi 25.1%. Kundi la benki la kimataifa "Goldman Sachs" linaamini kuwa, ifikapo mwaka 2050 uchumi wa nchi za BRICS utashindana na uchumi wa nchi tajiri zaidi duniani.

Jambo lingine muhimu ni kwamba BRICS inaweza kuwa mshindani mkubwa wa kundi la G7 linalojumuisha Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Uingereza. Baada ya nchi 6 mpya kujiunga na kundi la BRICS, mashirika ya habari ya Russia yaliandika katika uchanganuzi wa takwimu kwamba, jumla ya Pato la Taifa (GDP) la BRICS iliyostawi litakuwa takriban dola trilioni 65 katika suala la usawa wa uwezo wa kununua. Kwa utaratibu huo, sehemu ya kundi hili katika Pato la Taifa itaongezeka kutoka 31.5% ya sasa hadi 37%. Wakati huo huo, sehemu ya nchi zilizoendelea kiuchumi (G7) kwa sasa ni karibu 29.9%. Vilevile, nchi 11 za kundi la BRICS zitakuwa na eneo la kilomita mraba milioni 48.5, ambayo ni 36% ya eneo la dunia, na kiwango hicho ni zaidi ya mara mbili ya G7. Idadi jumla ya jamii ya watu wa nchi za kundi hilo la BRICS itafikia watu bilioni 3.6, ambayo ni 45% ya jamii ya dunia nzima na mara nne zaidi ya jamii ya G7.