Waliofariki katika tetemeko la ardhi nchini Afghanistan wapindukia 320
Oct 08, 2023 07:12 UTC
Idadi ya watu waliofariki dunia katika tetemeko la ardhi lililotokea jana nchini Afghanistan imepindukia 320.
Kwa mujibu wa IRNA, katika taarifa uliyotoa usiku wa kuamkia leo, Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa watu 320 wamefariki katika tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.3 kwa kipimo cha rishta lililotokea magharibi mwa Afghanistan hapo jana, na kwamba kuna uwezekano mamia ya watu wamejeruhiwa katika tetemeko hilo.
Kitovu cha zilzala hiyo kimetajwa kuwa ni kandokando ya mji wa Herat, ulioko kaskazini-magharibi mwa Afghanistan, na kina cha zilzala yenyewe ni kilomita 10. Ukali wa tetemeko hilo la ardhi ulikuwa mkubwa kiasi ambacho mtikisiko wake ulihisika pia katika baadhi ya sehemu za Iran, Turkmenistan na Uzbekistan.
Shirika la habari la Ufaransa AFP limenukuu kituo kimoja cha Utafiti wa Jiolojia cha Marekani kikitangaza kuwa: "kuna uwezekano idadi ya vifo ikawa kubwa sana."

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kabul umetoa mkono wa pole kwa jamaa za waliofariki na pamoja na majeruhi na waathirika wote wa tetemeko hilo la ardhi la Herat na kutangaza kuwa Iran iko tayari kupokea na kufikisha misaada ya kimataifa kwa waathirika wa tetemeko hilo katika fremu ya ushirikiano katika utoaji misaada ya kibinadamu na kulingana na taarifa ya Kazan, Russia na itaongeza huduma zake za mpakani kwa ajili ya utoaji misaada ya kibinadamu.
Wakati huohuo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kanani Chafi ameeleza masikitiko yake kwa kufariki dunia idadi kadhaa ya raia wa Afghanistan kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea mjini Herat na ametoa mkono wa pole kwa serikali ya muda ya Taliban na wananchi wa Afghanistan.../
Tags