Tarehe 7 Oktoba; kumbukumbu ya uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan
(last modified Tue, 10 Oct 2023 02:36:23 GMT )
Oct 10, 2023 02:36 UTC
  • Tarehe 7 Oktoba; kumbukumbu ya uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan

Miaka 22 iliyopita, Marekani iliishambulia nchi ya Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kurudisha amani nchini humo, jambo ambalo lilipelekea Waafghani kukabiliwa na matatizo na machungu mengi.

Jumamosi ya tarehe 7 Oktoba, ilikuwa ni siku ya kukumbuka mashambulizi ya mwaka 2001 ya Marekani dhidi ya Afghanistan na jinai za nchi hiyo na waitifaki wake huko Afghanistan. Marekani na waungaji mkono wake waliivamia nchi hiyo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kurudisha amani na usalama nchini humo.

Hatimaye, baada ya miaka 20 ya kuikalia kwa mabavu Afghanistan na kufanya jinai nyingi za kutisha pamoja na kuharibu miundombinu ya kiuchumi na kiafya, wanajeshi wa Marekani waliondoka katika nchi hiyo mwishoni mwa Agosti 2021 kwa aibu na madhila makubwa. Kundi la Taliban liliingia madarakani nchini Afghanistan katikati ya mwezi Augusti mwaka jana. Katika vita na uvamizi huo wa Marekani, takriban Waafghani laki mbili na nusu wakiwemo raia na waandishi habari, waliuawa.

Zabihullah Mujahid, Msemaji wa Serikali ya Taliban ya Afghanistan alisema Jumamosi katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kumbukumbu ya shambulio la Marekani dhidi ya nchi hiyo kwamba tarehe 7 Oktoba, imerekodiwa kama siku nyeusi katika historia ya nchi nchi hiyo, lakini baada ya kupita miaka ishirini, uvamizi huo wa Marekani ulishindwa. Zabihullah Mujahid alisema, siku hii nyeusi inathibitisha kwamba hakuna nchi yoyote yenye majivuno ambayo haijakuwa na ndoto ya kuivamia  Afghanistan.

Kushindwa Marekani Afghanistan

Vita vya miaka ishirini vya Marekani nchini Afghanistan na ambavyo vilikuwa ni vita vya muda mrefu zaidi vya nje ya Marekani kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Al-Qaeda na kumuua Osama bin Laden, kiongozi wa kundi hilo, lakini Bin Laden aliuawa  katika eneo la Abbottabad nchini Pakistan miaka kumi baada ya uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan.

Wakati huo, Hamid Karzai, aliyekuwa rais wakati huo nchini Afghanishtan alikosoa uvamizi wa Marekani nchini humo na kusema: Kwa kuuawa  Osama bin Laden nchini Pakistani,  imethibitika kuwa Afghanistan ni mhanga tu wa vita vinavyodaiwa kuwa ni vya kupambana na ugaidi. Hamid Karzai alisema: Maelfu ya Waafghanistan wasio na hatia kila siku huwa ni wahanga wa ugaidi na Jamii ya Kimataifa inayoongozwa na Marekani imefahamu ukweli huo baada ya miaka kumi.

Wakati huo huo, kwa amri ya Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani, idadi ya wanajeshi wa Marekani iliongezeka hadi 110,000 mwaka 2011, miaka kumi baada ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Afghanistan, idadi ambayo ilikuwa ya juu zaidi ya uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Afghanistan.

Katika vita hivyo, wanajeshi wa Marekani wapatao 2,500 waliuawa  na wengine zaidi ya 20,000  kujeruhiwa. Marekani ilitumia karibu dola trilioni mbili na nusu katika vita vyake vya miaka 20 nchini Afghanistan, ambao ilikuwa mzigo mzito kwa raia wa nchi hiyo kwa kadiri kwamba Mark Milley, Mkuu wa Majeshi ya Pamoja ya Marekani, alikiri kwamba vita vya nchi hiyo huko Afghanistan vilipelekea kushindwa wanajeshi wake nchini humo. Mark Milley, alisema katika mazungumzo na ABC News kuhusu kuondolewa wanajeshi wa Marekani kutoka Afghanistan, kuwa vita hivyo vya miaka 20 nchini Afghanistan havikuwa na mafanikio yoyote.

Alireza Kuhkan, mjumbe wa jopo la elimu la Chuo Kikuu cha Allameh Tabatabai, amesema kuhusiana na suala hilo kwamba kufeli kukubwa na kwa madhila Marekani katika karne ya 21 kulitimia kufuatia vita vyake vya kivamizi huko Afghanistan. Ilikuwa imepangwa kwamba Taliban, ambayo ambayo wakati huo ilikuwa madarakani huko Afghanistan ilitakiwa kuondolewa na Marekani, lakini baada ya kupita miaka ishirini Washington iliikabidhi Afghanistan kwa Taliban kwa mikono miwili na kuondoka nchini humo kwa madhila makubwa.

Uvamizi wa miaka 20 wa Marekani uliacha maafa na hasara zisizoweza kufidika kwa watu wa Afghanistan, yakiwemo mabomu ya kutegwa ardhini ambayo hayajalipuka, na ambayo hadi sasa yanaendelea kutoa roho za Waafghani wasio na hatia. Kuhusiana na suala hilo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) limetangaza katika ripoti yake kuwa asilimia 85 ya wahanga wa mabomu hayo ambayo hayajalipuka ni watoto wadogo. UNICEF imeongeza katika ujumbe huo kuwa Afghanistan ni mojawapo ya nchi zilizoathirika zaidi na silaha za vita.

Kilimo cha mipopi nchini Afghanistan kwa usimamizi wa askari wa Marekani

Kwa upande mwingine, zaidi ya watoto milioni tatu nchini Afghanistan wanakabiliwa na utapiamlo, watu milioni 15 wanahitaji chakula cha dharura na zaidi ya watu milioni 29 wanahitaji misaada ya kibinadamu. Kwa mujibu wa ripoti ya mashirika ya kimataifa, zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wa Afghanistan hawapati huduma za matibabu, afya wala chakula cha kutosha.

Pia, takriban watu milioni 19 nchini Afghanistan hawana uhakika wa kupata chakula na zaidi ya asilimia 90 wanaishi chini ya mstari wa umaskini, ambayo ni matokeo ya miaka ishirini ya uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan.

Matokeo mengine ya uvamizi huo ni uwepo wa mazao ya aina moja tu ya kilimo nchini Afghanistan na kuongezeka kwa kilimo cha mipopi, kwa kadiri kwamba suala hilo ili limeharibu sana uchumi wa nchi hiyo.

Kama zaidi ya dola trilioni mbili zilizotangazwa kutumika katika mashambulizi ya Marekani huko Afghanistan zingelitumika katika kuboresha miundombinu na maendeleo endelevu ya Afghanistan, watu wa nchi hiyo hawangelazimika kukimbia nchi yao wala kuvumilia machungu na matatizo ambayo hadi sasa yanawakabili.

Serikali ya Taliban pia inaweza kukubaliana na matakwa ya Jamii ya Kimataifa ya kuundwa nchini serikali shirikishi, kuwa na uhusiano mzuri na nchi mbalimbali na jirani, kuheshimu haki za raia na kuwapa wanawake haki zao za msingi, kuruhusu wanawake wafanye kazi na wasichana kusoma ili kuandaa mazingira ya kurudishwa usalama nchini, usalama ambao unaweza kutatua matatizo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya watu wa nchi hiyo.