CAIR: Israel imetangaza vita dhidi ya Uislamu kwa kuchoma moto Qur'ani
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limelaani vikali kitendo cha wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuchoma moto nakali za Qur'ani Tukufu katika Ukanda wa Gaza.
Nihad Awad, Mkurugenzi Mtendaji wa CAIR amesema katika taarifa kwamba, vitendo vya kufuru na kujipiga picha wakati wakichoma Qur’ani na vile vile kuharibu Misikiti kwa mara nyingine tena vinaonyesha kuwa vita vya Israel dhidi ya Wapalestina pia ni vita dhidi ya Uislamu.
Awad ameutaka utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani kulaani kuvunjiwa heshima matakatifu ya kidini ya Waislamu na kuacha kuupa silaha utawala wa Kizayuni ili kuulazimisha uhitimishe kampeni yake ya mauaji ya kimbari na kuwaua kwa njaa watu wa Gaza.
Picha zilizotolewa siku ya Ijumaa zilionyesha wanajeshi wa Israel wakivamia Msikiti wa Bani Saleh kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kisha kuchana chana na kuchoma nakala za Qur'ani Tukufu ndani ya Msikiti huo.
Kadhalika kundi hilo la kutetea haki za Waislamu na kiraia nchini Marekani limeeleza kusitikishwa na hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza, na kusisitiza kuwa jamii ya kimataifa ina wajibu wa kusimamisha mauaji ya watoto katika eneo hilo la Palestina lililozingirwa.
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limemtaka Biden alaani vitendo vya ugaidi wa kiserikali vinavyofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.