Oct 09, 2024 07:26 UTC
  • Marekani: Hatutaki kuingia vitani na Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani amesema kuwa, hawezi kuzungumzia uwezekano wa uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran lakini ana uhakika kwamba Washington haitaki kuingia vitani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Sabrina Singh amesema hayo mbele ya waandishi wa habari kwenye ofisi ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon, na kusema kuwa, nchi yake inaendelea kushauriana na utawala wa Kizayuni kuhusiana na jibu lake kwa kipigo cha makombora ambacho Israel imekipata kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini hakutoa ufafanuzi zaidi kuhusu mashauriano hayo. 

Operesheni ya Ahadi ya Kweli 2, Iran yaipa somo 'Israel'

Vile vile amesema kuwa viongozi wa Marekani na Israel wanawasiliana mara kwa mara, na wanaendelea kushauriana juu ya namna ya kujibu shambulizi la kulipiza kisasi lililofanywa na Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni chini ya kaulimbiu ya Ahadi ya Kweli 2, lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.

Tarehe Mosi Oktoba mwaka huu wa 2024, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliutia adabu utawala wa Kizayuni kwa kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya maeneo ya kijeshi na kiusalama ya Israel kwa kutumia makumi ya makombora iliyobuni na kutengeneza yenyewe Iran.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambalo ndilo lililoendesha operesheni hiyo ya kishujaa ilitangaza baada ya operesheni hiyo ya Ahadi ya Kweli 2, kwamba asilimia 90 ya makombora yake yamepiga kwa ustadi maeneo ya Wazayuni.