Russia yakanusha kuweko mazungumzo ya simu baina ya Putin na Trump
(last modified Tue, 12 Nov 2024 03:52:10 GMT )
Nov 12, 2024 03:52 UTC
  • Russia yakanusha kuweko mazungumzo ya simu baina ya Putin na Trump

Msemaji wa Ikulu ya Russia (Kremlin) amekanusha taarifa zilizodai kufanyika mazungumzo ya simu baina ya rais mteule wa Marekani Donald Trump na Rais Vladimir Putin wa Russia lakini wakati huo huo amesema kuwa, Rais Putin amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba hana tatizo na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi za Magharibi kama viongozi hao wataonesha nia ya kufanya hivyo.

Shirika la habari la Tasnim limeripoti habari hiyo na kumnukuu Dmitry Sergeyevich Peskov akisema hayo jana Jumatatu mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika baina ya Rais Vladimir Putin wa Russia na Donald Trump aliyetangazwa mshindi wa urais wa Marekani ikiwa ni kukanusha madai ya gazeti la Marekani la Washington Post lililodai kuwa viongozi hao wawili walifanya mazungumzo ya simu siku ya Alkhamisi.

Amesema, huu ndio mtindo wa uwasilishaji taarifa unaotumiwa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vinaonekana vikubwa duniani. Madai hayo ya gazeti la Marekani la Washington Post hayana ukweli wowote, ni uongo wa wazi na ni taarifa iliyopotoshwa kikamilifu.

Msemaji huyo wa Ikulu ya Russia ameongeza kuwa, ni kweli hivi sasa kuna ishara chanya za kufanyika mazungumzo baina ya Russia na Marekani lakini hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika baina ya Rais Putin na Trump. 

Amma kuhusiana na mazungumzo baina ya Russia na Ujerumani, Peskov amesema kuwa hivi sasa hakuna maandalizi wala ishara zozote za kufanyika kitu kama hicho.