Wamarekani Waarabu waliompigia kura Trump wamhimiza asimamishe vita Ghaza na Lebanon
(last modified Wed, 13 Nov 2024 11:47:16 GMT )
Nov 13, 2024 11:47 UTC
  • Wamarekani Waarabu waliompigia kura Trump wamhimiza asimamishe vita Ghaza na Lebanon

Wamarekani Waarabu waliompigia kura Donald Trump katika mji wenye Waislamu wengi wa Dearborn, jimboni Michigan wamemtaka rais huyo mteule atoe mwito wa kusitishwa vita mara moja huko Palestina na Lebanon.

Katika barua kiliyotuma kwenye mtandao wa Instagram, Chama cha Wafanyabiashara wa Marekani cha MENA, -kwa niaba ya Wamarekani wa Lebanon-, kimempongeza Trump kwa kurejea Ikulu ya White House na kusema, Dearborn "iligeuka rangi nyekundu katika uchaguzi huu wa urais," kikimaanisha rangi inayotumiwa kwenye machapisho ya vyombo vya habari na chama cha Republican.
 
Sehemu moja ya barua hiyo inasema: "kwa kujibu barua yako mashuhuri iliyotumwa kwa Wamarekani wenye asili ya Lebanon ya tarehe 26 Oktoba 2024, na kutokana na kuongezeka mashambulizi ya Israel baada ya uchaguzi wa Marekani, tunauhimiza uongozi wako na timu ya mpito kutumia ushawishi wako wa kisiasa kutaka vita visitishwe mara moja huko Lebanon na Palestina".
 
Barua hiyo ya Wamarekani Waarabu imeendelea kueleza: "hili linaendana na ahadi ya kuleta amani ya kudumu ambayo uliitoa katika barua na pia ana kwa ana wakati wa kutia saini Mikataba ya Amani".
Trump

Trump amekumbushwa kupitia barua hiyo kwamba, Wamarekani zaidi ya milioni 3.5 wa MENA, ambao baadhi yao wanaishi katika majimbo yenye ushindani mkali, wanajivunia kuchangia ushindi wake, hususan wa majimbo ya Michigan, Pennsylvania na Georgia; na kwamba mafanikio hayo ni ushuhuda wa usikivu wake, thamani na wasiwasi wa Wamarekani wa jamii ya MENA.

 
Ngome ya jadi ya Wademocrat ya mji wa Dearborn, jimboni Michigan, inayojulikana kama mji mkuu wa jamii ya Wamarekani Waarabu, ilitoa pigo la kushangaza kwa chama hicho katika uchaguzi wa rais wa Marekani kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono hujuma na mashambulio ya kinyama yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.
 
Jiji hilo, ambalo ni makao ya msikiti mkubwa zaidi wa Amerika Kaskazini na wenye wapiga kura Waislamu wapatao 250,000, lilishuhudia mabadiliko makubwa mwaka 2020, wakati Mdemokrati Joe Biden aliposhinda Michigan kwa takriban kura 150,000 na kumbwaga rais wa wakati huo Trump, ambaye alikuwa anamaliza muhula wake wa kwanza madarakani.../