WHO yautoa hofu ulimwengu kuhusu virusi vya HMPV
https://parstoday.ir/sw/news/world-i121192-who_yautoa_hofu_ulimwengu_kuhusu_virusi_vya_hmpv
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa ongezeko lililoripotiwa la wagonjwa walioathirika katika mfumo wao wa kupumua linalosababishwa na virusi vya Human Metapneumovirus (hMPV) huko China linaendana na mwelekeo wa msimu wa magonjwa ya kawaida ya kupumua, pamoja na mafua ambayo kwa kawaida hufikia kileleni wakati wa miezi ya baridi.
(last modified 2025-01-09T03:20:01+00:00 )
Jan 09, 2025 03:20 UTC
  • WHO yautoa hofu ulimwengu kuhusu virusi vya HMPV

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa ongezeko lililoripotiwa la wagonjwa walioathirika katika mfumo wao wa kupumua linalosababishwa na virusi vya Human Metapneumovirus (hMPV) huko China linaendana na mwelekeo wa msimu wa magonjwa ya kawaida ya kupumua, pamoja na mafua ambayo kwa kawaida hufikia kileleni wakati wa miezi ya baridi.

Kuenea kwa virusi hivyo nchini China kumezifanya nchi kadhaa, zikiwemo Nigeria na Afrika Kusini, kuimarisha ufuatiliaji katika viwanja vya ndege vikubwa vya kimataifa.

WHO imeeleza kuwa, hMPV ni virusi vya kawaida vinavyoathiri mfumo wa kupumua vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali duniani wakati wa msimu wa baridi hadi majira ya kuchipua, ingawa si nchi zote zinazojaribu na kuchapisha data mara kwa mara kuhusu mienendo ya virusi hivyo.

Shirika la Afya Duniani limeongeza kuwa, katika hali ambayo wakati mwingine watu hulazimika kulazwa hospitalini kwa kuathiriwa na mkamba au nimonia, watu wengi walioambukizwa virusi vya  hMPV huwa na dalili kama kukohoa, homa, maumivu ya koo n.k sawa na homa ya kawaida; na hupona baada ya siku chache.

WHO imependekeza watu wachukue tahadhari za kawaida ili kuzuia kuenea kwa vimelea vya magonjwa ya kupumua, haswa kwa watu walio hatarini wakati wa msimu wa baridi.