Alkhamisi, tarehe 04 Juni, 2026
Leo ni Alkhamisi tarehe 18 Dhulhija 1447 Hijria sawa na tarehe 04 Juni 2026.
Siku kama hii ya leo miaka 1437 iliyopita Mtume Muhammad (SAW) akiwa njia kurejea Madina kutoka kwenye safari yake ya mwisho ya Hija, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake.
Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum katika makutano ya njia ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume SAW alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui."
Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika Hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama. ***
Siku kama ya leo miaka 775 iliyopita, alifariki dunia Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hesabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran.
Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na aliasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran. Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi.
Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naaswiri’, ‘Awsaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat. **
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, tarehe 14 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia sawa na mwezi Juni 1989, Imam Ruhullah Musawi Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Ulimwengu wa Kiislamu uligubikwa na majonzi na huzuni kubwa kutokana na kutangazwa kifo cha Imam.
Imam Khomeini (M.A) alizaliwa tarehe Mosi mwezi wa Mehr mwaka 1281 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 24 Septemba 1902 katika mji wa Khomein ulioko katikati mwa Iran. Alianza kujishughulisha na siasa sambamba na masuala ya kielimu na kiutamaduni. Mapambano ya Imam dhidi ya utawala wa Shah na uingiliaji wa Marekani nchini Iran yalishtadi mwaka 1963 Miladia sawa na 1342 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, na kupelekea Imam kubaidishwa kwa miaka 13 nchini Iraq, Uturuki na Ufaransa. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi mwaka 1357 Hijiria Shamsia sawa na 1979 kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini (M.A).
Imam alibobea katika taaluma mbalimbali, na mbali na kuwasomesha wanafunzi wengi na kutoa hotuba nyingi za kihistoria, alikuwa pia mwandishi hodari wa vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake ni Tahrirul Wasilah, Kashful Asrar, Misbahul Hidayah, na Utawala wa Kiislamu na Uongozi wa Faqih. ***
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu lilimchagua Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuwa Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Uchaguzi huo ulifanyika masaa machache tu baada ya kufariki dunia Imam Khomeini (M.A) ambapo wasia wa Imam ulisomwa mbele ya hadhirina.
Hadi sasa Ayatullah Khamenei anaendeleza njia ya Imam Khomeini MA kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu na ameyaongoza Mapinduzi ya Kiislamu kwa hekima, tadbiri, uono wa mbali na ustahiki.
Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran inatoa salamu za rambirambi kwa mnasaba huu wa kukumbuka siku ya kuaga dunia hayati Imam Khomeini. ***
Tarehe 4 Juni mwaka 1989 yaani siku kama hii ya leo miaka 37 iliyopita, wanafunzi kadhaa wa vyuo vikuu vya China waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa na polisi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beijing.
Siku hiyo maelefu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya China walikuwa wamekusanyika katika Medani ya Tiananmen mjini Beijing, wenye maana ya 'Amani ya Mbinguni' wakitaka kuwepo mazingira ya wazi ya kisiasa nchini humo, kupunguzwa uwezo wa Chama cha Kisoshalisti, kuongezwa uwezo wa Bunge na kuchaguliwa wawakilishi wake.
Ingawa serikali ya China ilipiga marufuku maandamano hayo lakini wanafunzi waliendelea kukusanyika na mwishowe askari polisi na vikosi vya jeshi vikatumia silaha kuwakandamiza wanafunzi hao. ***
Leo ni Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji (International Day of Innocent Children Victims of Aggression).
Siku hiyo ilitangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1982 kwa ajili ya kushughulikia mashaka ya watoto wanaosumbuliwa na unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kiroho kufuatia hali mbaya ya watoto wa Palestina na Lebanon wanaosumbuliwa na ukatili wa utawala haramu wa Israel.
Ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto una sura na aina mbalimbali na unasababishwa na uzembe wa wazazi, viongozi wa kitaifa na kimataifa na makatili wasio na chembe ya huruma na wasiojali isipokuwa maslahi yao ya kimaada. ****