China yajibu mapigo kwa Marekani, yazitoza ushuru wa 34% bidhaa za nchi hiyo
Apr 05, 2025 02:36 UTC
China imetangaza kuwa itazitoza ushuru wa ziada wa 34% bidhaa zote zinazoagizwa kutoka Marekani, hatua inayoonekana kuwa ni ya kujibu mapigo kwa ushuru wa 34% ambao Rais Donald Trump ameziwekea bidhaa zinazozalishwa na nchi hiyo yenye uchumi wa pili mkubwa zaidi duniani.
Hii ni baada ya Washington kutangaza ushuru mpya wa ziada dhidi ya washirika na wapinzani wake.
Ushuru huo uliotangazwa na Beijing, ambao utaanza kutumika Alkhamisi ijayo, utaathiri bidhaa zote za Marekani zinazoingizwa China. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume ya Ushuru wa Forodha ya Baraza la Serikali.
Taarifa hiyo imeuita ushuru wa upande mmoja uliotangazwa na Marekani kuwa ni wa "kionevu," na kuongeza kuwa unakiuka sheria za biashara za kimataifa na kudhuru haki na maslahi ya China.
Siku ya Jumatano, China ilitozwa ushuru wa 34% wakati Trump alipotia saini amri ya utendaji ya uwekaji ushuru dhidi ya nchi nyingi duniani.
Kwa mujibu wa Wizara ya Biashara ya China, mbali na kuweka ushuru wa ziada, Beijing imepiga marufuku pia usafirishaji wa bidhaa zenye matumizi ya aina mbili kwa mashirika 16 ya Marekani na kuyaongeza makampuni 11 ya nchi hiyo kwenye "orodha ya taasisi zisizoaminika".
China imeanzisha pia uchunguzi wa bidhaa zenye bei ya kutupa kwa mirija ya matibabu ya CT (X-ray) kutoka Marekani na India na kuitaka Washington iondoe "mara moja" ushuru mpya ilioweka na kutatua mizozo yoyote iliyopo kupitia "mazungumzo ya haki na usawa" na washirika wake wa kibiashara.
Beijing imetangaza pia hatua za kudhibiti uuzaji nje ya nchi baadhi ya bidhaa zinazotokana na madimu adimu kupatikana duniani.../
Tags