Wafungwa Waislamu ‘wanalengwa’ na kukandamizwa nchini UK
(last modified Thu, 17 Apr 2025 02:30:24 GMT )
Apr 17, 2025 02:30 UTC
  • Wafungwa Waislamu ‘wanalengwa’ na kukandamizwa nchini UK

Shirika moja la kupigania haki za kijamii limefichua kwamba, wafungwa Waislamu nchini Uingereza wananyanyaswa na kuwekewa mbinyo, ikiwa ni pamoja na kupigwa marungu na kuwekewa vizuizi hasa katika magereza yenye Waislamu wengi.

Shirika la misaada ya kiraia la Maslaha, lilifanya uchunguzi katika magereza tisa yenye idadi kubwa ya Waislamu na kubaini kuwa wafungwa wanakandamizwa kwa njia mbali mbali, kwa kupigwa kwa fimbo, virungu na kufunwa  pingu zenye kuumiza.

Matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kuwa, katika vituo vinane kati ya tisa, kuna uwezekano mkubwa kwa askari magereza kutumia virungu, pingu zenye kubana na kuchubua mikono, na mbinu nyinginezo za kikatili dhidi ya wafungwa Waislamu ikilinganishwa na wafungwa wengine.

Shirika hilo pia limefichua kuhusu mbinu za kubana na kuwazuia kwa lazima wafungwa Waislamu magerezani humo, ikiwa ni pamoja na kuwavunja vidole gumba na vifundo vya mkono, pamoja na kukandamiza mishipa ya neva chini ya sikio.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa shirika la Maslaha, Raheel Mohammed, data hizo za kuogofya "zinaweka wazi uhalisia wa maisha" ya kila siku ya Waislamu walioko magerezani.

Takwimu za Wizara ya Sheria ya Uingereza zinaonyesha kuwa, kulikuwa na wafungwa Waislamu 15,594 nchini humo na Wales kufikia mwezi Septemba mwaka jana, ikiwa ni asilimia 18 ya jumla ya wafungwa wote, licha ya Waislamu kuwakilisha asilimia 6.5 tu ya jamii ya Waingereza.

Waislamu barani Ulaya wamekuwa wakikabiliwa na mawimbi ya vurugu, mashinikizo, hujuma na chuki dhidi yao kwa misingi ya imani yao. Baada ya kuanza vita vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Gaza Oktoba, 2023, ripoti zinaonesha ongezeko la asilimia 140 ya uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu katika nchi za bara hilo.