ICC yaifungulia mashtaka Hungary kwa kutomkamata Netanyahu
(last modified Fri, 18 Apr 2025 02:34:15 GMT )
Apr 18, 2025 02:34 UTC
  • ICC yaifungulia mashtaka Hungary kwa kutomkamata Netanyahu

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imefungua rasmi kesi dhidi ya Hungary baada ya serikali ya Budapest kukataa kutekeleza waranti wa ICC wa kumkamata waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu wakati wa ziara yake rasmi nchini humo mapema mwezi huu.

Mahakama hiyo ya mjini The Hague ilitangaza jana Jumatano kuamilisha Kifungu cha 87(7) cha Mkataba wa Roma; mkataba ulioasisi mahakama hiyo. Kifungu hicho kinaruhusu mahakama hiyo kuwasilisha faili la mataifa yasiyoipa ushirikiano kwa Bunge la Nchi Wanachama au Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hatua hiyo imekuja kutokana na Hungary kukataa kumkamata Netanyahu, anayesakwa na ICC kwa uhalifu wa kivita alioufanya katika vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza, wakati wa ziara yake ya Aprili 3-6 huko Budapest, ambapo alipokewa kwa taadhima na Waziri Mkuu, Viktor Orbán.

Kushindwa kwa Hungary kutii hati ya ICC ya kumkamata Netanyahu mapema mwezi huu kumeifanya mahakama hiyo kushutumu rasmi nchi hiyo kwa kukiuka majukumu yake kama iliyotia saini Mkataba wa Roma.

Serikali ya Orbán ilitangaza kuwa nchi hiyo itajitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, saa chache baada ya Netanyahu kuwasili mjini Budapest.

Netanyahu, ambaye kwa mujibu wa hati iliyotolewa na ICC, anatakiwa akamatwe na kukabidhiwa kwa mahakama hiyo akikabiliwa na tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza, kwa kiburi na jeuri aliamua kufanya ziara rasmi ya kuitembelea Hungary ambayo ni nchi mwanachama wa mahakama hiyo.

Kukaidi Hungary kutekeleza agizo la kumkamata Netanyahu, ikiwa ni nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya na ambayo imetia saini Mkataba wa Roma, kumekosolewa vikali ndani na nje ya nchi hiyo.