Russia yaituhumu Ulaya na NATO kuwa zinajiandaa kwa makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi
(last modified Wed, 07 May 2025 06:35:53 GMT )
May 07, 2025 06:35 UTC
  • Russia yaituhumu Ulaya na NATO kuwa zinajiandaa kwa makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi

Katibu wa Baraza la Usalama la Russia, Sergei Shoigu, amelituhumu shirika la kijeshi la nchi za Magharibi, NATO na Umoja wa Ulaya kuwa zinaandaa mzozo wa moja kwa moja wa kijeshi na Moscow.

Katika makala yake kwenye gazeti la Rossiyskaya Gazeta, Shoigu amesema: "Wakichochewa na kuungwa mkono na London na Paris, wasomi wa Ulaya wanaendelea kutoa matamshi makali kuhusu haja ya kutoa kipigo cha kimkakati dhidi ya Russia.

Ameongeza kuwa NATO na Umoja wa Ulaya zimeanzisha mipango inayolenga kuzitayarisha nchi za Magharibi kwa makabiliano ya kijeshi ya moja kwa moja na nchi yake, akizitaja hatua hizo kuwa za "uchokozi."

Awali, Rais wa Russia, Vladimir Putin alizishutumu nchi za Magharibi kuwa zinajaribu kumchochea atumie silaha za nyuklia nchini Ukraine.

"Walitaka kutuchokoza, walitaka kutusukuma kufanya makosa," Putin alisema katika matamshi yake yaliyojumuishwa kwenye waraka wa televisheni ya serikali uliohusu miaka 25 akiwa madarakani.

Rais wa Russia aliongeza kuwa, hata hivyo, hakuna haja ya kutumia silaha za nyuklia, na kusema, "Natumai hakutakuwa na haja ya jambo hilo katika siku zijazo pia."