Wahanga wa mafuriko ya Texas, Marekani yaongezeka hadi watu 50
Kufuatia mafuriko makubwa yaliyotokea katika jimbo la Texas nchini Marekani, mamlaka za eneo hilo zimetangaza kuwa idadi ya waliofariki dunia imepindukia 50 na wengine wasiopungua 29 hawajulikani waliko.
Maafisa wa jimbo la Texas wametangaza kuwa jumla ya vifo vilivyosababishwa na mafuriko katika jimbo hilo imefikia watu wasiopungua 50, ikiwa ni vifo 43 katika Kaunti ya Kerr na vitatu katika Kaunti ya Burnett.
Mafuriko makubwa katika Kaunti ya Kerr, Texas, Mystic Camp, yamesomba kambi ya wasichana wa Kikristo na idadi kadhaa ya wasichana wa kituo hicho ambao wametoweka inaongezeka.
Gavana wa Texas, Greg Abbott, ametangaza hali ya hatari na kuipanua hadi Kaunti ya Travis.
Eneo la Texas Hill Country la Marekani limekuwa likishuhudia vifo na maafa tangu Ijumaa, Julai 4. Mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo imesababisha mafuriko makubwa na kuwalazimisha waokoaji kutumia boti na helikopta kuokoa watu walionaswa.
Licha ya juhudi kubwa za uokoaji, hadi sasa idadi isiyojulikana ya watu bado imetoweka na operesheni za dharura zinaendelea.
Rais wa Marekani Donald Trump alisema: "Mafuriko haya yameibua mshtuko na maafa ya kutisha."