Kremlin: Hatuna habari kuhusu mkutano wa Putin, Trump, Xi
Msemaji wa Ikulu ya Russia (Kremlin) amesema hana ufahamu wowote kuhusu taarifa kwamba Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin, mwenzake wa Marekani, Donald Trump na kiongozi wa China Xi Jinping watakutana nchini China karibuni hivi.
Msemaji wa Rais wa Russia, Dmitry Peskov amesema Ikulu ya Kremlin haifahamu mpango wa Rais wa Russia, Vladimir Putin, mwenzake wa Marekani, Donald Trump, na kiongozi wa China Xi Jinping kukutana nchini China pambizoni mwa sherehe za kuadhimisha miaka 80 ya ushindi katika Vita vya Mapambano dhidi ya uvamizi wa Japan.
"Hatujui chochote kuhusu uwezekano kama huo," Peskov amesisitiza katika mahojiano na shirika la habari la TASS, juu ya ripoti za uwezekano wa kufanyika mkutano huo kama zilivyoripotiwa na The Times.
Gazeti hilo la Uingereza limeripoti kuwa, Rais Xi anataka viongozi wa Marekani na Russia wakutane mwezi Septemba mwaka huu, katika hafla ya kumbukumbu za vita hivyo vya kujihami vya China.
China itaadhimisha kumbukizi ya miaka 80 ya ushindi wake katika Vita vya Mapambano, na Rais Putin tayari amealikwa kuzuru nchi hiyo ya Asia Mashariki kuhudhuria sherehe hizo.
Haijabainika ikiwa Donald Trump atasafiri kwa ndege hadi Beijing kuhudhuria hafla hiyo, ziara ambayo gazeti hilo lilisema kuna uwezekano mdogo kufanyika.