Umoja wa Mataifa wahimiza usuluhishi wa amani wa migogoro
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128682-umoja_wa_mataifa_wahimiza_usuluhishi_wa_amani_wa_migogoro
Nchi 193 za Umoja wa Mataifa zimehimizwa kuongeza nguvu zaidi katika usuluhishi wa amani wa migogoro duniani.
(last modified 2025-07-23T23:18:09+00:00 )
Jul 23, 2025 23:18 UTC
  • Umoja wa Mataifa wahimiza usuluhishi wa amani wa migogoro

Nchi 193 za Umoja wa Mataifa zimehimizwa kuongeza nguvu zaidi katika usuluhishi wa amani wa migogoro duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amani inahitaji sana kwa sasa. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limezihimiza nchi 193 wanachama wa umoja huo zitumie njia zote zinazowezekana kusuluhisha migogoro kwa njia ya amani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema muelekeo huo unahitajika sana kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameashiria hali ya kutisha katika Ukanda wa Gaza na mizozo inayoendelea nchini Ukraine, Sudan, Haiti na Myanmar. Akihimiza juu ya kufanyika jitihada zaidi kutafuta amani ya dunia, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameliambia Baraza la Usalama kwamba, kote duniani kunashuhudiwa hali ya kutoheshimu wala kuzingatia sheria ya kimataifa pamoja na mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema:" Kushindwa huku kutimiza wajibu wa kimataifa kunakuja wakati kukishuhudiwa migawanyiko na migogoro ya kilimwengu inayoongezeka. Na gharama yake ni kubwa hasa kwa maisha ya binaadamu, kusambaratisha jamii na kuharibu mustakabali wetu." Wakati huo huo, Baraza la Usalama siku ya Jumanne lilipasisha azimio likizitaka nchi wanachama wote "kutumia ipasavyo" taratibu za utatuzi wa mizozo ka amani kama ilivyoainishwa katika mkataba wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na "mazungumzo, uchunguzi, upatanishi, maridhiano, usuluhishi, usuluhishi kupitia utaratibu wa kisheria," na njia nyingine zozote za amani wanazochagua.